WANANCHI WAPONGEZA UDHIBITI WA MAFURIKO MTO KIKULETWA


MOSHI-KILIMANJARO.

WANANCHI wa Kitongoji cha Kiruani, Kijiji cha Chemchem, Kata ya Arusha Chini, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wameipongeza Serikali kupitia Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB) kwa kufanikiwa kudhibiti mafuriko yaliyokuwa yakijitokeza mara kwa mara katika Mto Kikuletwa na kusababisha hasara kubwa kwa makazi, mashamba na miundombinu.

Wakazi wa eneo hilo wamesema hatua ya kuondoa tope na kurejesha mkondo wa asili wa mto huo imeondoa hofu ya mafuriko yaliyokuwa yakiwakumba kila msimu wa mvua za masika na kuwawezesha kuendelea na shughuli za kilimo kwa utulivu.


Mkazi wa eneo hilo, Saimon Molell, alisema Serikali ilichukua hatua kwa wakati kwa kufika eneo hilo na kuanza kuondoa tope na udongo uliokuwa umejaa katika Mto Kikuletwa, hali iliyokuwa ikisababisha maji kupoteza mkondo wake na kuingia katika makazi ya wananchi.

"Kuondolewa kwa tope hilo kumepunguza kwa kiasi kikubwa athari za mafuriko yaliyokuwa yakitokea mara kwa mara na kutuharibia makazi na mashamba yetu," alisema Molell.

Mjumbe wa Jumuiya ya Watumiaji Mto Kikuletwa, Alex Joseph Mgaya, alisema kabla ya utekelezaji wa mradi huo, mto huo ulikuwa umepoteza mkondo wake wa asili na kusababisha maji kuelekea kwenye mashamba na makazi ya wananchi, jambo lililosababisha hasara kubwa kwa wakulima.

Alisema baada ya Bodi ya Maji Bonde la Pangani kuanza kazi ya kuondoa tope na kurejesha mkondo wa mto huo, mafuriko yamepungua kwa kiwango kikubwa na wananchi sasa wana matumaini ya kuishi bila hofu.



"Kwa kweli tunaishukuru Serikali. Sasa tunaishi kwa matumaini makubwa na bila hofu ya mafuriko yaliyokuwa yakitokea kila msimu wa mvua," alisema.

Mgaya aliomba Serikali iendelee kutoa elimu kuhusu usimamizi wa rasilimali za maji na kuimarisha ushirikiano na wananchi ili kuhakikisha changamoto za mafuriko zinadhibitiwa kikamilifu.

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Kiruani, Dinis Mazigo, alisema hapo awali wakulima walikuwa wakipata hasara kubwa kutokana na maji ya Mto Kikuletwa kuacha mkondo wake na kuelekea kwenye makazi na mashamba yao.

Alisema baada ya mto huo kurejeshwa katika mkondo wake wa asili, wakulima wameanza kunufaika na mazao yao kutokana na kuwa na uhakika wa kuvuna bila hofu ya mafuriko.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Chemchem, Abdallah Musa Mpendu, alisema mto huo ulipoteza mkondo wake wa asili na kusababisha uharibifu mkubwa wa makazi, mashamba na miundombinu.

"Tunaushukuru sana uongozi wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kudhibiti mto huu na kurejesha maji katika mkondo wake wa asili," alisema.

Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani, Mhandisi Segule Segule, alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau ilianza kutekeleza mradi wa kudhibiti mafuriko katika eneo hilo lenye urefu wa kilomita 3.5 kwa lengo la kurejesha mkondo wa asili wa Mto Kikuletwa na kulinda maisha na mali za wananchi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani, Mhandisi Ruth Koya, aliipongeza timu inayotekeleza mradi huo na kuwataka wananchi kuendelea kuzingatia sheria na taratibu za matumizi ya rasilimali za maji ili kulinda vyanzo vya maji na kupunguza athari za mafuriko.

Alisema hadi sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia kilomita 2.56 kati ya kilomita 3.5, sawa na asilimia 73.14, huku kazi zilizobaki zikiendelea kukamilishwa kwa lengo la kuimarisha ulinzi wa makazi ya wananchi, mashamba na miundombinu.












Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.