MOSHI-KILIMANJARO.
MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nur Babu, amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, kuwatafuta, kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wanufaika wote wa mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri kupitia makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambao wameshindwa kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.
Babu alitoa agizo hilo Juni 30,2026, wakati wa hafla ya kukabidhi mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.1 kwa vikundi 82 vya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.
Alisema wako baadhi ya wanufaika walikopeshwa fedha hizo tangu mwaka 2023, lakini hadi sasa hawajarejesha mikopo hiyo, jambo linalokwamisha lengo la Serikali la kuwafikia wanufaika wengine.
"Wale wote ambao hawajarudisha mikopo waliyopewa tangu mwaka 2023, Mkuu wa Wilaya nakuagiza watafutwe popote walipo, wakamatwe na wafikishwe mahakamani. Lazima na sisi tuwe kama mabenki yanavyofanya kwa wadaiwa sugu. Mtu akishindwa kurejesha mkopo kwa wakati, hatua za kisheria zichukuliwe ili fedha za umma zilindwe," alisema Babu.
Alisisitiza kuwa fedha hizo ni za wananchi, hivyo lazima zirejeshwe ili ziendelee kuwanufaisha wengine wanaohitaji mitaji ya kuanzisha au kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.
Babu alisema kurejeshwa kwa mikopo hiyo pia kutaiwezesha Manispaa ya Moshi kuongeza uwezo wa kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara na huduma nyingine muhimu kwa wananchi.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, alisema dirisha la mikopo ya asilimia 10 lililoanzishwa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan limekuwa fursa muhimu ya kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi kwa kuongeza uzalishaji na kukuza biashara zao.
Akisoma taarifa ya utoaji wa mikopo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe, alisema tangu Rais Dk. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, halmashauri hiyo imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 7 kwa jumla ya vikundi 840.
Alifafanua kuwa kati ya vikundi hivyo, vikundi 549 vya wanawake vilipatiwa mikopo ya shilingi bilioni 3.8, vikundi 221 vya vijana vikapatiwa shilingi bilioni 3, huku vikundi 70 vya watu wenye ulemavu vikikopeshwa jumla ya shilingi milioni 215.5.
Nasombe alisema katika mwaka wa fedha 2025/2026, kupitia robo ya tatu na ya nne, Halmashauri imeidhinisha utoaji wa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.1 kwa vikundi 82. Kati ya hivyo, vikundi 42 vya wanawake vitapatiwa shilingi milioni 463.3, vikundi 26 vya vijana vitapatiwa shilingi milioni 635.9, huku vikundi 14 vya watu wenye ulemavu vikitengewa shilingi milioni 61.9.













