MANGI MKUU WA WAGWENO ASIMIKWA RASMI

                                       
                                                      MSANGENI-UGWENO.

Serikali mkoani Kilimanjaro imepongeza hatua ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kurejesha rasmi mfumo wa uongozi wa kimila, hatua iliyotajwa kuwa na mchango mkubwa katika kulinda na kuenzi utamaduni wa Kitanzania.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, katika hafla ya kusimikwa kwa Mangi Mkuu wa Ugweno, Ahmed Rajab Minja wa Tatu, sherehe iliyofanyika katika Kijiji cha Msangeni, Tarafa ya Ugweno, na kuhudhuriwa na viongozi wa kimila, viongozi wa serikali, wanazuoni na wananchi kutoka sehemu mbalimbali za mkoa wa Kilimanjaro.

Alisema kurejeshwa kwa uchifu ni hatua ya kurejesha heshima ya jamii na kuimarisha mshikamano wa wananchi huku akisema kuwa kuwepo kwa Kitala cha Kimila kutawapa wazee nafasi rasmi ya kukutana, kujadiliana na kushiriki katika ujenzi wa jamii na kwamba viongozi hao wa kimila watasaidia kueneza maendeleo, kupatanisha watu na hata kuimarisha utii wa sheri

"Serikali inatambua na kuenzi nafasi ya viongozi wa kimila katika kuimarisha mshikamano wa kijamii, kukuza maadili, na kulinda historia yetu, tunamshukuru sana Rais Samia kwa uamuzi wake wa busara wa kurejesha uchifu, bila kuenzi mila na tamaduni zetu, tunapoteza dira ya taifa na kuanza kuiga mifumo isiyo yetu," alisema DC Munkunda.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Majid Mwanga, alimpongeza Mangi Ahmed Rajab Minja wa tatu, kwa kusimikwa, akieleza kuwa anatarajia ataunganisha wakazi wote wa Wilaya ya Mwanga bila kujali wanatoka maeneo ya Tambarare, Usangi au Ugweno.       

                                         

Awali, akisoma risala kwa mgeni rasmi, Mratibu wa Kamati ya Maandalizi ya sherehe hizo, Prof. Mark Leveri, alieleza kuwa Mangi atakuwa na majukumu makuu matano, ikiwemo, kuwa mlinzi wa mila na tamaduni za jamii ya Ugweno, kielelezo cha umoja wa watu, mshauri kwa serikali za mitaa, mpatanishi wa migogoro ya kifamilia na koo kwa kutumia busara za jadi na kuhamasisha ushiriki wa jamii katika miradi ya maendeleo. 

                                             

Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo John Yoen Msuya (maarufu kama Lumumba) alieleza kuwa Mangi hupatikana kupitia familia maalum za kifalme ambazo ni chimbuko la kihistoria la uongozi wa Wamangi, na kwamba hatua ya kurejeshwa kwa uchifu inaleta heshima kubwa kwa jamii ya Ugweno na kizazi kijacho.

Akizungumza kwa mara ya kwanza akiwa Mangi Mkuu wa Ugweno, Ahmed Rajab Minja, aliahidi kushirikiana kwa karibu na serikali katika kuimarisha mshikamano wa kijamii, kukuza maadili, na kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi, hususan vijana.

“Jukumu mlilonikabidhi ni kubwa, lakini kwa msaada wa serikali na wazee, tutaweza kulirudisha eneo letu katika misingi ya utamaduni na maendeleo, nitakuwa daraja kati ya serikali na wananchi,” alisema Mangi Ahmed.

Alisema moja ya changamoto kubwa inayolikumba eneo hilo ni mmomonyoko wa maadili miongoni mwa vijana, akibainisha kuwa matumizi ya dawa za kulevya, bangi na mirungi vimeathiri uwezo wa vijana kushiriki kikamilifu katika uzalishaji.

“Vijana wengi hawajishughulishi tena na kazi, asubuhi badala ya kunywa chai, wanakimbilia kuvuta bangi au ‘kutoa lock’. Kazi yangu ya kwanza itakuwa kuunda baraza la Washiri kutoka kila Kata ili tusaidiane na serikali kutatua tatizo hili,” alisema.

Kusimikwa kwa Mangi Mkuu wa Ugweno kunatazamwa kama hatua ya kihistoria katika kurejesha utambulisho wa jamii, huku serikali ikiahidi kuendelea kushirikiana na viongozi wa kimila kama sehemu ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo na kudumisha amani.

                                       









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.