Katika hafla ya kihistoria na yenye uzito wa kipekee kwa jamii ya Wagweno, Ahmed Rajab Minja, maarufu kama Mavanja, alitawazwa rasmi kuwa Mangi Mkuu wa III wa Wagweno, na hivyo kuwa Mangi wa 21 kutoka ukoo wa kifalme wa Wasuya, ukoo ulioongoza Ugweno tangu karne ya 17.
Tukio hilo limefanyika Jumamosi Juni 14,2025 katika Kijiji cha Msangeni, Kata ya Msangeni Tarafa ya Ugweno, Wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro, baada ya miaka 63 tangu kufutwa kwa mfumo rasmi wa Umangi mwaka 1963, chini ya Serikali ya Tanganyika ya wakati huo, iliyoongozwa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mangi Ahmed Rajab Minja ni mtoto wa Mangi wa mwisho wa Ugweno, Rajab Minja Kikome, ambaye alikuwa Mangi hadi mfumo huo ulipositishwa rasmi.
Urithi wa Ufalme wa Ugweno.
Historia ya utawala wa Ugweno inaanzia enzi za ukoo wa Washana, waliotawala kuanzia nusu ya pili ya milenia ya kwanza hadi karne ya 16. Kuanzia karne ya 17, uongozi ulichukuliwa na ukoo wa Wasuya, uliodumu hadi 1963. Katika kipindi hicho, Mangi Mkuu alikuwa mhimili wa uhusiano kati ya utawala, mila na jamii.
Ahmed Rajab Minja, sasa Mangi Mkuu wa III, ni mrithi halali wa ukoo wa Wasuya, akifuatilia nasaba ya kifalme inayoanzia kwa Mangi Angovi, na kisha kwa mwanawe Mranga Angovi, ambaye anatajwa kuleta mfumo wa utawala wa kipekee wenye mvumo wa kisasa, uliodhihirika katika uongozi wa Wagweno hadi leo.
Wasifu wa Mangi Mkuu Minja III
Mangi Ahmed Rajab Minja alizaliwa Mei 12, 1949, katika kijiji cha Msangeni, Ugweno. Alimaliza elimu ya msingi mwaka 1965, na kuhitimu sekondari mwaka 1969. Kisha alijiunga na Chuo cha BTC kilichopo Nairobi, Kenya, ambako alipata Diploma ya Masoko na Mauzo.
Katika maisha ya kitaaluma, alifanya kazi katika taasisi mbalimbali za Jumuiya ya Afrika Mashariki kama mtaalamu wa masoko, zikiwemo East African Literature Bureau, East African Publications Ltd, na CEA Publications Ltd.
Alishiriki maonyesho ya kimataifa kama London Book Week na Frankfurt Book Fair kati ya 1973 na 1985, na alisafiri kote Afrika Mashariki akieneza ushawishi wa usambazaji wa vitabu.
Kuanzia 1986 hadi 2002, alianzisha kampuni ya Mavanja Snacks (AR), na pia alikuwa Mkurugenzi wa Arusha Integrated School, zaidi ya hapo, aliongoza Umoja wa Wagweno waishio Arusha, akiendeleza harakati za kijamii, utamaduni, na maendeleo ya jamii ya Wagweno walioko nje ya nyumbani.
Kazi na Dhamira ya Utawala Mpya.
Katika utawala wake mpya, Mangi Mkuu Ahmed Rajab Minja III anatarajiwa kuwa kiunganishi kati ya Serikali na jamii ya Ugweno, akisisitiza maendeleo yanayozingatia mila, desturi, na utambulisho wa kitamaduni wa Wagweno, licha ya kuwa kiongozi wa kimila, ataheshimu katiba na sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Majukumu yake yatahusisha: Moja ikiwa ni kulinda na kuendeleza mila na desturi za jadi za Wagweno, Kukuza mshikamano, amani na maelewano ndani ya jamii, Kusaidia usuluhishi wa migogoro kwa njia za jadi, Kuwezesha maendeleo ya kijamii, kielimu, na kiuchumi, Kuwakilisha sauti ya Wagweno katika ngazi mbalimbali za uongozi wa kitaifa.
Kutawazwa kwa Mangi Mkuu Ahmed Rajab Minja III ni tukio la kihistoria linaloashiria kuhuishwa kwa urithi wa kifalme wa jamii ya Wagweno, kwa njia ya amani, maelewano, na kwa kuzingatia sheria za kisasa, ikiwa ni hatua ya kulinda utambulisho wa jamii, huku ikifungua ukurasa mpya wa matumaini kwa vizazi vya sasa na vijavyo.