MOSHI-KILIMANJARO.
VIONGOZI na watumishi wa umma, mkoa wa Kilimanjaro wametakiwa kuzingatia misingi ya utawala bora na kutambua kuwa kuzuia vitendo vya rushwa, hususan katika utekelezaji wa programu na miradi ya maendeleo, ni jukumu la kila Mtanzania na si la Serikali au TAKUKURU pekee.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, wakati akifungua Warsha ya Wadau wa Usimamizi wa Programu na miradi ya maendeleo iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.
Amesema Serikali inaendelea kutenga fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hivyo viongozi na watumishi wa umma wanapaswa kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa uadilifu, uwazi na kwa manufaa ya wananchi ili miradi hiyo ifikie malengo yaliyokusudiwa.
Aidha, amewataka wasimamizi wa miradi kutekeleza majukumu yao kwa weledi, kuzingatia sheria na kuepuka migongano ya maslahi, akisisitiza kuwa maendeleo ya Mkoa wa Kilimanjaro yanategemea uwajibikaji, ushirikiano na usimamizi mzuri wa rasilimali za umma.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa, ameishukuru TAKUKURU kwa kuandaa warsha hiyo, akisema itawaongezea uwezo wataalamu na watendaji katika kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi.
Naye Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro, Musa Chaulo, amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026 taasisi hiyo ilifuatilia miradi ya maendeleo 329 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 55.2, ambapo miradi 130 ilibainika kuwa na mapungufu mbalimbali, huku miradi 124 ikifanyiwa marekebisho na kukamilika kwa wakati baada ya ushauri wa TAKUKURU.
Aidha amesema lengo la warsha hiyo ni kuwajengea uwezo wadau wa usimamizi wa miradi ya maendeleo ili kuondoa viashiria vya rushwa, kuboresha utekelezaji wa miradi na kuhakikisha fedha za umma zinatumika ipasavyo kwa manufaa ya wananchi.



















