BONANZA LA KKKT LAVUTA ZAIDI YA VIJANA 500 KUSAKA VIPAJI

MOSHI, KILIMANJARO.

ZAIDI ya vijana 500 kutoka maeneo mbalimbali ya Jimbo la Vunjo, wamekusanyika katika bonanza la michezo la Vijana wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), lililofanyika Marangu Mashariki, huku likitajwa kuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji vya michezo na kufungua fursa za maendeleo ya kiuchumi kwa vijana.

Akifungua rasmi bonanza hilo, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Enock Koola, amesema michezo imeendelea kuwa sekta muhimu inayochangia maendeleo ya taifa kwa kuibua vipaji, kuzalisha ajira na kuwawezesha vijana kujenga maisha yao kupitia taaluma mbalimbali za michezo.

Amesema mbali na kutoa burudani, michezo hufundisha nidhamu, mshikamano, ushindani wa haki na uzalendo, huku ikitoa nafasi kwa vijana wenye vipaji kufikia ngazi za juu za ushindani ndani na nje ya nchi.

"Michezo ni njia muhimu ya kuwajenga vijana kimwili, kiakili na kiuchumi, tunahitaji kuendelea kuwekeza katika vipaji vyao ili viwe chanzo cha ajira, kipato na maendeleo ya jamii," amesema Koola.

Mbunge huyo amewataka vijana kuendelea kumcha Mungu, kuishi kwa maadili mema na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuharibu ndoto zao, ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya, uhalifu na makundi yanayochochea uvunjifu wa amani.

Kuhusu uwezeshaji wa vijana, Koola amesema ofisi yake inaendelea kutekeleza programu mbalimbali za kuwainua vijana, kiuchumi kupitia mafunzo ya ufugaji wa kuku wa kibiashara, ufugaji wa ng'ombe wa maziwa, ufugaji wa samaki, kilimo cha kisasa na ujasiriamali.

Ameongeza kuwa ofisi yake pia imewaajiri vijana wanaosaidia wenzao kuunda vikundi vya kiuchumi, kuandaa nyaraka za kuomba mikopo ya Halmashauri isiyo na riba pamoja na kuwaunganisha na taasisi za kifedha zinazotoa mikopo yenye masharti nafuu.

Kwa mujibu wa Koola, uwekezaji kwa vijana kupitia michezo, elimu na ujasiriamali ni njia bora ya kuandaa kizazi chenye uwezo wa kujitegemea na kuchangia maendeleo ya taifa.

Bonanza hilo lilihusisha michezo mbalimbali pamoja na ibada na maombi, likiwa na lengo la kuimarisha umoja, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa vijana wa KKKT Jimbo la Kilimanjaro Mashariki, huku likitoa nafasi ya kutambua na kuendeleza vipaji vinavyoweza kung'ara katika michezo ya ushindani.






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.