MILIONI 10 ZAPIGANIWA KOOLA VUNJO CUP 2026


MOSHI, KILIMANJARO

KITITA cha shilingi milioni 10 pamoja na kikombe kinatarajiwa kuibua ushindani mkubwa kwa timu 16 zitakazoshiriki mashindano ya Koola Vunjo Cup 2026, yatakayozinduliwa rasmi Agosti 9 katika Viwanja vya Polisi Himo, wilayani Moshi.

Mshindi wa kwanza wa mashindano hayo ataondoka na shilingi milioni tano pamoja na kikombe, huku mshindi wa pili akijinyakulia shilingi milioni tatu na mshindi wa tatu shilingi milioni mbili.

Mbali na zawadi za timu, waandaaji wameandaa tuzo mbalimbali za kutambua ubora wa washiriki. Golikipa bora na mfungaji bora kila mmoja atazawadiwa shilingi 300,000, timu yenye nidhamu itapata shilingi 400,000, kocha bora shilingi 100,000, chipukizi bora shilingi 200,000, huku kundi bora la mashabiki likiondoka na shilingi 300,000.

Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea uzinduzi wa mashindano hayo, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Iddi Mfinanga, amesema maandalizi yanaendelea vizuri na timu 16 zimethibitisha kushiriki katika mashindano hayo yanayolenga kuibua vipaji vya soka na kuhamasisha maendeleo ya michezo kwa vijana wa Vunjo.

Amesema dirisha la usajili wa wachezaji lilifunguliwa Julai 13 na litafungwa Julai 31 mwaka huu ili kutoa nafasi kwa timu kukamilisha maandalizi yao kabla ya kuanza kwa mashindano.

Mfinanga amesema Agosti Mosi kutafanyika zoezi la kugawa vifaa vya michezo kwa timu zote zitakazoshiriki, ambapo kila timu itapatiwa mipira miwili na seti mbili za jezi kwa lengo la kuboresha ushindani na kuongeza hadhi ya mashindano.

Ameongeza kuwa Koola Vunjo Cup-2026 imeandaliwa si kwa lengo la kupata bingwa pekee, bali pia kuibua vipaji vya vijana vitakavyoweza kupata nafasi katika ngazi za juu za soka, sambamba na kuimarisha mshikamano na kukuza uchumi kupitia shughuli mbalimbali zinazozunguka mashindano hayo.

Kwa mujibu wa ratiba, fainali ya Koola Vunjo Cup 2026 itachezwa Oktoba 25 katika Viwanja vya Polisi Himo, huku waandaaji wakitarajia mashindano hayo kuvutia mashabiki wengi na kuwa jukwaa la kuendeleza vipaji vya soka katika Jimbo la Vunjo na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.