CCM; YAWATAKA MADIWANI KUELEZA WANANCHI MAFANIKIO YA SERIKALI YA DKT. SAMIA

MOSHI-KILIMANJARO.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi Vijijini kimewataka madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, kuendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu miradi na huduma mbalimbali zilizotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Sirili Mushi, alipokuwa akizungumza katika kikao cha Baraza la Hoja za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Amesema ni muhimu madiwani wakatumia nafasi zao kuwaeleza wananchi mafanikio yaliyopatikana katika kata wanazoziongoza ili wananchi waone matokeo ya utekelezaji wa Ilani ya chama na kazi zinazofanywa na serikali

Amesema katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa ikiwemo ujenzi wa madarasa, vituo vya afya, zahanati, barabara pamoja na huduma nyingine za kijamii ambazo zimeendelea kuboresha maisha ya wananchi.

Aidha ameipongeza Kamati ya Fedha ya Halmashauri kwa kusimamia vizuri matumizi ya fedha za umma na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi.

Pia amewapongeza wabunge wa majimbo ya Moshi Vijijini, Morris Makoi na Enock Koola, kwa kuendelea kuwatetea na kuwasemea wananchi wao bungeni, hatua ambayo amesema imechangia kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo wa Wilaya , amewataka viongozi wa chama na serikali kuendelea kuimarisha umoja na ushirikiano, akisisitiza kuwa katika ukaguzi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, makatibu wa CCM wa kata washirikishwe ili kuongeza uwazi, ushirikiano na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi hiyo.









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.