HALMASHAURI YA MOSHI, YATAKIWA KUFUNGA HOJA ZA CAG, KUENDELEA KUPATA HATI SAFI

MOSHI-KILIMANJARO.

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Moshi kwa kufanikiwa kupata hati safi katika ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025, huku akiitaka kuhakikisha hoja zote zinazobainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinafanyiwa kazi na kufungwa kwa wakati.

Babu alitoa kauli hiyo wakati akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi kilichoketi kwa ajili ya kupokea na kujadili Ripoti ya CAG.

Amesema kupata hati safi ni hatua muhimu inayodhihirisha kuimarika kwa usimamizi wa fedha za umma, lakini mafanikio hayo yanapaswa kuambatana na utekelezaji wa mapendekezo yote ya ukaguzi ili kuzuia kujirudia kwa kasoro zilizobainishwa.

Aidha amewataka madiwani kuisimamia kikamilifu halmashauri hiyo kwa kuhakikisha mifumo ya uwajibikaji inaendelea kuimarishwa na matumizi ya fedha za umma yanafanyika kwa kuzingatia sheria na taratibu za Serikali.

Pia ameiagiza menejimenti ya halmashauri kusimamia kwa karibu urejeshwaji wa mikopo iliyotolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili fedha hizo ziendelee kuwanufaisha wananchi wengine na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa, amewataka watumishi wa halmashauri kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya Serikali ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Naye Mkaguzi Mkuu wa Nje wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Kilimanjaro, Wenslaus Kyaruzi, amesema Halmashauri ya Wilaya ya Moshi imefanikiwa kupata hati safi kutokana na kuboresha mifumo ya usimamizi wa fedha, kutekeleza mapendekezo ya ukaguzi na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma.

Amesema kuwa hatua hizo zimechangia kuongezeka kwa uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za halmashauri, jambo ambalo limeiwezesha kupata matokeo mazuri katika ukaguzi wa mwaka wa fedha 2024/2025.











Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.