WAWEKEZAJI WATAKIWA KUTUMIA FURSA ZA MABORESHO YA MAZINGIRA YA BIASHARA YANAYOFANYWA NA SERIKALI

MOSHI- KILIMANJARO


SERIKALI imepongezwa kwa kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kupitia uimarishaji wa miundombinu, maboresho ya sera mbalimbali pamoja na kuondoa vikwazo vinavyozuia ukuaji wa sekta binafsi, hatua ambayo imeendelea kuvutia wawekezaji kuanzisha na kupanua biashara zao katika maeneo mbalimbali nchin.

Hayo yalisemwa Julai 6,2027 na Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, wakati akizindua jengo jipya la Vifaa vya ujenzi la Kampuni ya Tujenge Pamoja Hardware Co. Ltd mjini Moshi.

Alisema Serikali inaendelea kutambua mchango mkubwa wa sekta binafsi katika kuzalisha ajira, kuongeza mapato ya Serikali na kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa.

Alisema; kuendelea kukua kwa sekta binafsi ni msingi muhimu wa maendeleo ya uchumi wa Moshi, akibainisha kuwa jengo hilo jipya ni ishara ya mafanikio ya kampuni pamoja na dhamira yake ya kuendelea kuwahudumia wananchi kwa kuwapatia vifaa vya ujenzi vya kisasa na vinavyokidhi viwango vya ubora.


Alisema kituo hicho kitatoa huduma ya vifaa mbalimbali vya ujenzi ikiwemo saruji, nondo, mabati, rangi, vifaa vya umeme na vifaa vya maji, hivyo kuwaondolea wananchi, wakandarasi, mafundi na taasisi usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kutafuta bidhaa hizo.

Aidha, aliwahimiza wakazi wa Moshi Mjini kuendelea kuwaunga mkono wafanyabiashara wanaowekeza katika eneo hilo kwa kununua bidhaa na huduma zao, akisema kufanya hivyo kutasaidia kukuza uchumi wa ndani, kuongeza fursa za ajira na kuimarisha maendeleo ya jamii.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Tujenge Pamoja Hardware Co. Ltd, Benson John Kirarika, alisema uwekezaji huo unalenga kusogeza huduma za vifaa vya ujenzi karibu zaidi na wananchi na kuwawezesha kupata bidhaa bora kwa urahisi.

Aidha aliiomba Serikali kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara, ikiwemo kurahisisha upatikanaji wa mikopo ili waweze kupanua biashara zao na kuongeza uwekezaji.

Uzinduzi wa jengo hilo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa vifaa vya ujenzi katika mji wa Moshi na maeneo ya jirani, sambamba na kuimarisha mchango wa sekta binafsi katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Kilimanjaro.
















Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.