MOSHI-KILIMANJARO.

Taarifa hiyo imetolewa Julai 3,2026 na Mratibu wa mashindano hayo, Mwalimu Japhet Mpande, wakati akizungumza na Kisena Blogs, ambapo alisema hafla ya uzinduzi itaanza saa 12:00 jioni katika Viwanja vya Hugos vilivyopo mjini Moshi.
Mpande alisema kuwa baada ya uzinduzi huo kutafanyika zoezi la kupiga kura litakalopanga ratiba ya mechi za mashindano, ikiwemo kuzipata timu mbili zitakazofungua rasmi Zuberi Cup 2026 katika mchezo wa Julai 11 utakaochezwa kwenye Viwanja vya Reli Njoro.
Alieleza kuwa maandalizi ya mashindano hayo yanaendelea vizuri, huku waandaaji wakijipanga kuhakikisha yanakuwa ya ushindani mkubwa na yanazingatia misingi ya haki na uwazi kwa timu zote zitakazoshiriki.
Kwa mujibu wa Mpande, Zuberi Cup ilianzishwa mwaka 2021 ikiwa na lengo la kukuza vipaji vya vijana kupitia mchezo wa soka, na tangu wakati huo imeendelea kukua kwa kasi kwa kuvutia idadi kubwa ya timu kila mwaka, hali iliyoongeza ushindani na kutoa fursa kwa wachezaji wengi kuonyesha uwezo wao.
Aliongeza kuwa waandaaji wanawakaribisha wadau wa michezo, viongozi na wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia uzinduzi huo pamoja na kuunga mkono juhudi za kuendeleza soka la vijana katika Mkoa wa Kilimanjaro.







