MOSHI-KILIMANJARO.
MBUNGE wa Jimbo la Vunjo, Enock Zadock Koola, ametimiza ahadi yake kwa wananchi baada ya kununua mitambo ya kisasa ya ujenzi na ukarabati wa barabara itakayosaidia kuboresha miundombinu katika jimbo hilo na maeneo mengine ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, huku Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa mitambo hiyo.
Mitambo hiyo, ambayo itanufaisha wananchi wa kata mbalimbali za Jimbo la Vunjo, inatarajiwa kuzinduliwa Julai 14, mwaka huu, katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Moshi zilizopo Sango, Kata ya Kimochi.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Idd Mfinanga, amesema ununuzi wa mitambo hiyo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Mbunge Koola wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, baada ya wananchi kueleza changamoto kubwa ya ubovu wa barabara zilizokuwa zikikwamisha shughuli za maendeleo.
Mfinanga; amesema mitambo hiyo itatumika kufungua barabara mpya, kufanya matengenezo ya mara kwa mara pamoja na ukarabati wa barabara zilizoharibika, hatua itakayosaidia kuhakikisha barabara za vijijini zinapitika katika kipindi chote cha mwaka.
Amesema uwepo wa mitambo hiyo utaondoa utegemezi wa kukodi vifaa kutoka maeneo mengine, jambo ambalo limekuwa likisababisha ucheleweshaji wa matengenezo ya barabara na kuongeza gharama za utekelezaji wa miradi ya miundombinu.
Kwa mujibu wa Mfinanga, uboreshaji wa barabara utarahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo, kupunguza gharama za usafiri, kuongeza upatikanaji wa huduma za kijamii na kuchochea shughuli za uchumi katika Jimbo la Vunjo na maeneo ya jirani.
Kwa muda mrefu wananchi wa jimbo hilo wamekuwa wakilalamikia ubovu wa miundombinu ya barabara, hali iliyokuwa ikisababisha magari kuharibika mara kwa mara, ongezeko la gharama za usafiri na ugumu wa kuwafikia wananchi kwa huduma mbalimbali, hususan wakati wa mvua.
Baadhi ya wakulima wameeleza kuwa wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kusafirisha mazao yao kwenda sokoni kutokana na barabara na madaraja kuharibika, hali inayowaletea hasara na kupunguza kipato.
"Tunapata shida sana kusafirisha mazao yetu. Barabara zimeharibika na madaraja mengine hayapitiki. Tunaamini mitambo hii italeta mabadiliko makubwa kwa sababu sasa matengenezo yatafanyika kwa wakati," amesema mmoja wa wakazi wa Jimbo la Vunjo.
Wananchi wameeleza matumaini kuwa uwekezaji huo utafungua fursa mpya za maendeleo, kuboresha huduma za usafiri na kuharakisha shughuli za kiuchumi, huku wakimpongeza Mbunge Koola kwa kutekeleza ahadi yake ya kuboresha miundombinu ya barabara.
Hafla ya uzinduzi wa mitambo hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, madiwani, viongozi wa vyama vya siasa na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Jimbo la Vunjo.



