MOSHI-KILIMANJARO.
AFISA wa Bodi ya Ligi Tanzania, Abdul Mgude, amesema mashindano ya Zuberi Cup yamekuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji vya soka kwa vijana, hususan katika kipindi hiki ambacho dirisha la usajili limefunguliwa kwa ligi mbalimbali nchini.
Mgude alitoa kauli hiyo Julai 11, 2026, wakati wa uzinduzi wa msimu wa sita wa mashindano hayo uliofanyika katika Uwanja wa Railway, Njoro, Manispaa ya Moshi.
Alisema mashindano hayo yanatoa nafasi kwa wachezaji kuonyesha uwezo wao mbele ya makocha, wasaka vipaji na viongozi wa klabu mbalimbali.
Alieleza kuwa kutokana na kufunguliwa kwa dirisha la usajili katika Ligi Kuu Tanzania Bara, Championship na First League, mashindano hayo yanakuwa fursa adhimu kwa vijana kujitangaza na kupata nafasi ya kusajiliwa na timu mbalimbali nchini.
"Baadhi ya wasaka vipaji na viongozi wa klabu wapo hapa kwa ajili ya kufuatilia wachezaji, hivyo, vijana wanapaswa kutumia mashindano haya kuonyesha uwezo wao na kujitengenezea nafasi ya kucheza katika ligi mbalimbali za Tanzania," alisema Mgude.
Aidha, alisema Bodi ya Ligi itaendelea kushirikiana na waandaaji wa Zuberi Cup ili kuhakikisha mashindano hayo yanazidi kuwa bora na yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya soka nchini.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kilimanjaro (KRFA), Abdallah Thabit, alimpongeza mdhamini wa mashindano hayo Zuberi Abdallah Kidumo, kwa juhudi zake za kuboresha miundombinu ya viwanja vya michezo, akisema hatua hiyo imeongeza hadhi ya mashindano na kutoa mazingira bora kwa wachezaji.
Thabit alisema miaka iliyopita viwanja vingi vilikuwa vya vumbi na vilikosa ubora unaohitajika, lakini sasa maboresho yaliyofanyika yamechangia kuongeza usalama wa wachezaji, ubora wa mchezo na kuwavutia wadau wengi zaidi wa soka.
Naye Mwenyekiti wa UWT Moshi Mjini, Theresia Komba, alimpongeza mdhamini wa mashindano hayo, Meya wa Manispaa ya Moshi, Zuberi Abdallah Kidumo, kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutumia michezo kama nyenzo ya kujenga afya za vijana, kuimarisha umoja na kuibua vipaji.
Komba alisema uboreshaji wa viwanja mbalimbali vya michezo utawapa vijana mazingira salama na rafiki ya kucheza soka, tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo walicheza katika viwanja vya vumbi, hali iliyokuwa ikiathiri kiwango cha mchezo na afya zao.
Alisisitiza kuwa Zuberi Cup imeendelea kuwa moja ya mashindano makubwa ya ngazi ya jamii yanayochochea maendeleo ya soka mkoani Kilimanjaro na kutoa matumaini kwa vijana wengi wanaotamani kufikia ndoto zao za kucheza soka la ushindani nchini.








