MOSHI-KILIMANJARO.
MPIRA wa miguu umeendelea kuthibitisha kuwa si mchezo wa dakika 90 pekee, bali ni nyenzo muhimu ya kuunganisha jamii, kukuza uchumi na kuibua vipaji vya vijana.
Hali hiyo ndiyo inayoifanya Zuberi Cup Tournament Season 6 kuwa miongoni mwa mashindano ya soka yanayozidi kupata heshima katika Mkoa wa Kilimanjaro kutokana na mchango wake kwa maendeleo ya michezo na jamii kwa ujumla.
Serikali imewahakikishia wananchi wa Wilaya ya Moshi kuwa kutakuwa na amani, utulivu na ulinzi wa kutosha ili kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika katika mazingira salama kuanzia mchezo wa ufunguzi hadi fainali.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, wakati wa uzinduzi rasmi wa Zuberi Cup Msimu wa sita, uliofanyika katika Viwanja vya Hugos mjini Moshi.
Mnzava alisema Serikali inatambua mchango wa mashindano hayo katika maendeleo ya vijana na ndiyo sababu itaendelea kuhakikisha usalama unakuwepo wakati wote wa mashindano.
Alisisitiza kuwa mtu yeyote atakayejaribu kuvuruga utulivu wa mashindano hayo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, huku akiwataka mashabiki na wadau wa michezo kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kudumisha amani ambayo ndiyo msingi wa mafanikio ya mashindano yoyote.
Mnzava alimpongeza Mwanzilishi na Mdhamini wa Mashindano hayo, Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, kwa kujitolea kutumia rasilimali zake binafsi kuwekeza katika maendeleo ya michezo, hasa kuibua vipaji vya vijana vinavyoweza kufungua milango ya ajira na kucheza soka la ushindani.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya, alisema mashindano hayo ya Zuberi Cup imekuwa daraja la kuwaunganisha wananchi kutoka kata, vijiji na maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kilimanjaro, huku ikijenga mshikamano, urafiki na uzalendo kupitia michezo.
Alieleza kuwa mbali na ushindani wa uwanjani, mashindano hayo yamekuwa yakichochea mzunguko wa fedha katika Manispaa ya Moshi,ambapo wachezaji hupata nafasi za kuonekana na kusajiliwa na timu mbalimbali, huku wafanyabiashara wadogo wakiongeza kipato kupitia biashara zinazofanyika viwanjani.
"Kunapokuwa na mashindano makubwa kama haya, kuna ongezeko la shughuli za kiuchumi. Wauzaji wa chakula, vinywaji, matunda, vifaa vya michezo, pamoja na sekta ya usafiri kama bodaboda, bajaji na magari ya abiria wote hunufaika," alisema Mnzava.
Aliongeza kuwa michezo pia ni silaha muhimu katika kupambana na uhalifu miongoni mwa vijana, kwani vijana wanapokuwa na shughuli za michezo hupunguza uwezekano wa kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya, bangi, mirungi pamoja na vitendo vingine vya uhalifu.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu huyo Wilaya ya Moshi , alimpongeza Mhandisi Kidumo kwa kusaidia jitihada za Serikali za kuwaweka vijana katika mazingira yenye tija kupitia michezo.
Aidha, Mnzava alizitaka timu zote zitakazoshiriki mashindano hayo kucheza kwa nidhamu, kufuata sheria 17 za mchezo wa mpira wa miguu na kuheshimu maamuzi ya waamuzi.
Katika hafla hiyo Mnzava alisema bingwa atakayepatikana anapaswa kukubaliwa kwa ushindi wa halali, huku timu ambazo hazitafanikiwa zikijipanga kwa mashindano yajayo.
Katika hatua nyingine, Mnzava alisema atazungumza na baadhi ya klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwemo Pamba FC na Coastal Union FC, ili kutuma wawakilishi wao kufuatilia mashindano hayo kwa lengo la kutafuta wachezaji wenye vipaji watakaoweza kusajiliwa katika msimu ujao wa ligi.
Kwa upande wake, Mwanzilishi na Mdhamini wa mashindano hayo, Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, alisema Zuberi Cup imeendelea kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kimichezo katika Manispaa ya Moshi.
Alisema kila siku ya mchezo imekuwa ikiwapa mamia ya wafanyabiashara fursa ya kuongeza kipato kupitia biashara mbalimbali zinazofanyika viwanjani, hali inayochochea uchumi wa wananchi wa kawaida.
Mbali na biashara hizo, alisema sekta ya usafirishaji nayo imeendelea kunufaika ambapo madereva wa bodaboda, bajaji na magari ya abiria hupata wateja wengi wanaokwenda na kurudi viwanjani wakati wa mashindano.
Kidumo alisema mwaka huu kila timu itakayoshiriki itapatiwa mipira miwili ili kuongeza hamasa ya maendeleo ya soka la msingi. Pia ameahidi kuendelea kushirikiana na wadau wengine wa michezo ili kusaidia timu zenye uhitaji wa vifaa mbalimbali.
Alisema ujenzi wa uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu unaoendelea ndani ya Manispaa ya Moshi utakuwa na manufaa makubwa ikiwa vijana wataendelea kushiriki mashindano yanayowapa nafasi ya kuonyesha vipaji vyao.
Kwa mujibu wa Kidumo, Zuberi Cup imezalisha ajira nyingi zisizo rasmi kupitia waamuzi, waratibu wa mashindano, wahudumu wa huduma ya kwanza wa Red Cross, walinzi, watangazaji wa viwanjani, wapiga picha, wapiga video na watoa huduma wengine mbalimbali.
Aidha, alisema mashindano hayo yamechangia kuboresha miundombinu ya viwanja vya michezo, ikiwemo Viwanja vya Railway, Mandela na Njoro ambavyo vimeboreshwa kwa kupandwa nyasi na kuwekwa mazingira rafiki kwa wachezaji pamoja na mashabiki.
Mbali na michezo, Zuberi Cup imeendelea kuwa jukwaa la utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu afya, utunzaji wa mazingira, usalama barabarani, kupinga matumizi ya dawa za kulevya, kupinga ukatili wa kijinsia pamoja na masuala mengine muhimu ya kijamii.
Baadhi ya wachezaji waliohudhuria uzinduzi huo walimpongeza Mhandisi Kidumo kwa kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya soka la vijana. Walisema uboreshaji wa viwanja na kuongezeka kwa mashindano ya ushindani kumewapa nafasi ya kuonyesha uwezo wao mbele ya makocha na viongozi wa klabu mbalimbali.
Kwa miaka sita sasa, Zuberi Cup imeendelea kujijengea sifa kama moja ya mashindano makubwa ya soka ngazi ya jamii katika Mkoa wa Kilimanjaro
Mashindano hayo si tu yanazalisha mabingwa, bali pia yanazalisha ajira, yanakuza uchumi, yanajenga mshikamano na kuwapa vijana matumaini ya kufikia ndoto zao kupitia mpira wa miguu.
Ikiwa kasi hiyo itaendelea na wadau wengi zaidi wakaunga mkono juhudi hizo, Zuberi Cup inaweza kuwa moja ya vyanzo vikubwa vya kuzalisha vipaji vitakavyoitumikia Tanzania katika ligi za ndani, timu za taifa na hata soka la kimataifa. Huo ndio uthibitisho kwamba michezo, inapowekezwa ipasavyo, ni injini ya maendeleo ya jamii na uchumi.

















