MOSHI-KILIMANJARO.
VIJANA wanaochipukia katika soka wametakiwa kujituma maozoezini sambamba na kuwa na nidhamu ili waweze kufikia malengo yao ya kuwa wachezaji wenye viwango vya kutumainiwa na timu wanazochezea.
Ushauri huo umetolewa Julai 8,2026 na mchezaji wa Simba Selemani Mwalimu wakati wa uzinduzi wa uwanja wa soka uliokarabatiwa wa Nelson Mandela ulioko kata ya Bomambuzi, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, ambapo pamoja na mambo mengine alizawadiwa vifaa vya michezo na uongozi wa Kamati ya maandalizi ya michuano ya kila mwaka ya kombe la Zuberi Cup.
“Mimi hadi kufikia hatua hii niliyonayo, nilijituma haswa kwenye eneo la mazoezi ambapo nilikuwa nikiamka saa 11 alfajiri na wenzangu kuja kufanya mazoezi kwenye uwanja huu unaozinduliwa leo”, alisema na kuongeza, mazoezi mengine ambayo ni ya ngazi ya klabu yalikuwa yakifanyika jioni.
Aliongeza, “Mchezaji ukizingatia haya sambamba na kuwa na nidhamu ya hali ya juu ni lazima utapata mafanikio makubwa kwenye ulimwengu wa soka kiasi cha kuwa mchezaji wa kulipwa wa kimataifa”.
Alisema wachezaji wote wanaoonekana kung’ara ndani na nje ya nchi mafanikio yao yamepatikana baada ya kujituma zaidi kwenye mazoezi na kisha kuhamishia kujituma huko kwenye michuano mbalimbali ya soka ya kiushindani.
“Ili kufanikiwa cha kwanza ni kumweka Mwenyezi Mungu mbele maana yeye ni Mkubwa tunachohitajika kuwa nacho sisi ni Imani; baada ya hapo lazima mtu uzingatie mazoezi sambamba na kuwa na nidhamu ya hali ya juu”, alisema.
Akizungumzia uzinduzi huo, Mdhamini wa mashindano hayo na Meya wa Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo alisema maboresha ya uwanja umelenga kuwavutia vijana wengi zaidi kushiriki michezo na hivyo kuepuka kushiriki maswala ambayo hayazingatii maadili mema na kwamba mipango iliyoko ni kuendelea kuboresha viwanja mbalimbali manispaa ya Moshi.
“Tulianza na uwanja wa Railway, ulipo Kata ya Njoro , mwaka huu tumeuboresha huu wa Nelson Mandela uliopo kata ya Bombambuzi, mipango ya baadaye ni kuboresha viwanja kwenye kata zingine ili vijana wapate maeneo ya kufanya mazoezi na kushiriki michezo mingine kwa ukaribu zaidi”, alisema.
Kwa upande wa Zawadi alizotoa Mdhamini wa mashindano hayo kwa wachezaji Seleman Mwalimu, Ramadhan na Chobwedo wa timu ya TRA ya mkoani Tabora, Kidumo alisema kuwa kamati hiyo imechukua uamuzi huo kwa heshima ambayo wachezaji hao walionyesha kwa michuano hiyo ya kombe la Zuberi cup.
“Kwa wachezaji ambao tayari wameng’ara kwa kiasi kikubwa na kupata heshima kwenye medani ya soka kuchukua uamuzi wa kuitangaza michuano hii ambayo ni ya kawaida kabisa ni heshima kubwa ambayo haingefaa kuicha ipite bila kuonyesha shukrani zetu”, alisema.
Aliongeza, “Kwa mchezaji ambaye amefikia hatua ambayo wamefikia vijana wetu wawili hawa wangeweza kunyamaza tu lakini wameona ni vyema waitangaze michuano ambayo itaweza kuibua vipaji kama ilivyokuwa kwao ndiyo maana na sisi tukaamua kuwapa Zawadi zinaoendana na mchezo wa soka”.
Alisema kuwa Zawadi hizo ni viatu vya soka ambavyo ni aina ya vile vinavyotumika kwenye michauno inayoendelea ya kombe la dunia mwaka huu, pamoja na mpira wa miguu ambao pia nia aina ya ile inayotumika kwenye michuano ya kombe la dunia mwaka huu.















