AZANIA BENKI YAKABIDHI MIPIRA 10 KUIUNGA MKONO ZUBERI CUP

MOSHI-KILIMANJARO.

BENKI ya AZANIA imekabidhi mipira 10 kwa Kamati ya Mashindano ya Zuberi Cup ikiwa ni sehemu ya kutekeleza ahadi yake ya kudhamini mashindano hayo yanayoendelea katika viwanja mbalimbali vya Manispaa ya Moshi.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo, Meneja wa Azania Benki Tawi la Moshi, Yusuph Lenga, alisema benki hiyo imeendelea kutekeleza ahadi zake kwa lengo la kuunga mkono maendeleo ya michezo na kukuza vipaji vya vijana.

"Tupo hapa kutekeleza moja ya ahadi tuliyoitoa kwa Kamati ya Mashindano ya Zuberi Cup, kama mnavyofahamu, Azania Benki ni miongoni mwa wadhamini wa mashindano haya, huku mdhamini mkuu akiwa Meya wa Manispaa ya Moshi, Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, sisi kama Azania Benki tutaendelea kushirikiana na kamati kuhakikisha mashindano haya yanafanikiwa," alisema Lenga.

Alisema mipira hiyo itagawiwa katika viwanja vinavyotumika kwa mashindano ili kuhakikisha mechi zote zinafanyika katika mazingira bora na kwamba huo ni mwanzo wa utekelezaji wa ahadi mbalimbali ambazo benki hiyo ilizitoa kwa kamati ya mashindano.

Lenga alisema kuanzia hatua ya 16 Bora, Azania Benki itaanza kutoa zawadi kwa washindi wa tuzo mbalimbali zikiwemo mchezaji bora, kipa bora, kocha bora, mfungaji bora pamoja na timu itakayokuwa na nidhamu ya hali ya juu.

Aidha, aliwataka wanamichezo, mashabiki na wananchi kwa ujumla kuendelea kuiunga mkono Azania Benki kwa kufungua akaunti na kutumia huduma zake, akisema hatua hiyo itaongeza uwezo wa benki kuendelea kudhamini na kuendeleza michezo katika jamii.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Zuberi Cup, Mwalimu Japhet Mpande, aliishukuru Azania Benki kwa kutimiza ahadi yake, akisema msaada huo utasaidia kuongeza ubora wa mashindano.

"Tunawashukuru sana Azania Benki kwa kutekeleza ahadi yao, mipira hii itatumika katika viwanja vyetu vya mashindano na itachangia kuendesha ligi kwa ufanisi zaidi. Ushirikiano huu unatoa motisha kwa kamati na timu zinazoshiriki," alisema Mpande.












Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.