CHAUMA YAWAHAMASISHA WATANZANIA KUSHIRIKI UCHAGUZI MKUU, YAONYA DHIDI YA KUSUSIA


                                                MOSHI-KILIMANJARO.

Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA), Salim Mwalimu, ametoa wito kwa Watanzania kote nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu wa Rais, Wabunge na Madiwani, akisisitiza kuwa mabadiliko ya kweli hayawezi kupatikana kwa wananchi kubaki majumbani.

Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye eneo la Stendi ya Vumbi, Manispaa ya Moshi, Salim Mwalimu amesema ushiriki wa wananchi katika uchaguzi ni kiini cha demokrasia na silaha kuu ya kuhakikisha mabadiliko ya kiuongozi na kimaendeleo yanatimia.

“Twendeni tukashiriki uchaguzi, lakini tukumbuke, hakuna mabadiliko yatakayotokea kwa sisi kukaa majumbani. Ushindi haupatikani mezani, bali uwanjani, kwenye sanduku la kura. Siku ya ushindi ni siku ya mapambano,” alisema Mwalimu huku akishangiliwa na wafuasi wa chama hicho.

Salim Mwalimu alisema CHAUMA kimejipanga kuingia katika uchaguzi huo kwa nguvu mpya, kikiwa na lengo la kusimamisha wagombea katika nafasi mbalimbali ikiwemo ubunge na udiwani, na kwamba chama hicho kitaendelea kuwa jukwaa la kuwasemea Watanzania wa kawaida.

“Tutasimamisha wagombea wa madiwani, wagombea wa ubunge hapa Manispaa ya Moshi na maeneo mengine nchini kote. CHAUMA haitabaki pembeni, tutakuwa na sauti ndani ya mabaraza ya uamuzi,” aliongeza.

Katika mkutano huo, Mwalimu alikemea vikali tabia ya baadhi ya vyama vya siasa kususia chaguzi, akisema hatua hiyo ni sawa na kujitenga na wananchi na kukwepa wajibu wa kuongoza harakati za kidemokrasia.

“Kuacha kushiriki uchaguzi kwa chama kikuu cha siasa ni sawa na kuijaribu sumu kwa kuonja. Ukishindwa kujiamini uwanjani, usitegemee ushindi kutoka pembeni. Demokrasia inahitaji ujasiri, si manung’uniko,” alisema.

Ameongeza kuwa wananchi wa Tanzania hawapaswi kukata tamaa na mchakato wa uchaguzi, bali wanapaswa kuutumia kama fursa ya kuwawajibisha viongozi na kuchagua uongozi unaoendana na matarajio yao ya maendeleo.

Akihitimisha hotuba yake, Salim Mwalimu aliahidi kuwa kampeni za CHAUMA zitajikita katika hoja, sera na kushirikisha wananchi, huku chama hicho kikiahidi kuwa sauti ya wanyonge na daraja la matumaini kwa wale waliopoteza imani na mfumo wa kisiasa wa sasa.

Uchaguzi Mkuu wa Tanzania unatarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, huku vyama vya siasa vikiendelea na maandalizi mbalimbali, ikiwemo kutoa wito wa ushiriki mkubwa kwa wananchi na kuhimiza kampeni za amani.

Kwa upande wake, Kaimu Makamu Mwenyekiti wa CHAUMMA, Devotha Minja, aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi mkuu ujao, akieleza kuwa matatizo ya kijamii, kiuchumi na kiutawala hayawezi kuondoka bila wananchi kufanya maamuzi sahihi kupitia sanduku la kura.

"Twendeni tukashiriki uchaguzi, matatizo tuliyonayo, ukosefu wa huduma bora, ukandamizaji wa demokrasia, kukosekana kwa uwajibikaji, hayawezi kuondoka kama hatutachagua viongozi makini, viongozi wanaotoka kwa wananchi na wanaowajibika kwa wananchi," alisema Devotha.

Aidha, alifichua kuwa uamuzi wake wa kuondoka ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kujiunga na CHAUMMA umetokana na tofauti za kimsimamo kuhusu ushiriki katika uchaguzi mkuu.

“Ilipofika mwezi Aprili mwaka huu, Chadema walikataa kwenda kusaini kwa maandalizi ya uchaguzi, wakasema hawako tayari kushiriki..nilipoyaona hayo, na mimi nikagoma nikaamua kuachana nao, nikaelekea CHAUMMA, chama ambacho kiko tayari kuongeza mapambano na kuleta maendeleo kwa wananchi,” alisema Devotha.

Alisisitiza kuwa wananchi hawawezi kuendelea kuwa watazamaji katika masuala yanayogusa maisha yao ya kila siku, na kwamba ni wajibu wa kila Mtanzania kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuamua hatma ya taifa.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.