UJENZI WA UWANJA WA KISASA WA RAILWAY NJORO WAWAPA MATUMAINI VIJANA

                                                          MOSHI.

Kwa muda mrefu, vijana katika Kata ya Njoro, Manispaa ya Moshi, wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi katika harakati zao za kucheza soka, hususan kutokana na miundombinu duni ya viwanja.

Wengi walilazimika kucheza kwenye maeneo yasiyo rasmi, yenye mashimo, vumbi au mawe, hali iliyosababisha majeraha ya mara kwa mara na kuwakatisha tamaa baadhi yao kuendelea na michezo.

“Wakati mwingine tulicheza kwa hofu, unaweza kuanguka na kuvunjika mguu, halafu hakuna hata msaada wa haraka, tulikuwa tunapenda mpira lakini mazingira yalikuwa magumu sana,” alisema mmoja wa vijana waliowahi kushiriki mashindano hayo".

Hata hivyo, matumaini yamerudi upya baada ya Diwani wa Kata ya Njoro ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Zuberi Abdallah Kidumo, kuchukua hatua ya kujenga uwanja wa kisasa katika eneo hilo. 

Uwanja huo wa Railway upo kata ya Njoro, umejengwa kwa viwango vya kisasa, ukiwa na nyasi za kupandwa, vizuizi vya usalama, na miundombinu mingine inayowezesha vijana kucheza katika mazingira salama na ya kuvutia.

Akizungumza Mstahiki Meya Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo alisema “Niliona mateso wanayopitia vijana wetu na nikajua ni lazima kuchukua hatua, michezo ni ajira, ni afya, na ni fursa ya maendeleo, hatutaki vipaji vipotee kwa sababu ya ukosefu wa miundombinu ndipo nikaamua kujenga uwanja huu kwa kushirikiana na wadau wengine niliowakimbilia na kunishika mkono.”alisema Mhandisi Kidumo.

Hatua hii inatajwa kupokelewa kwa shangwe na wakazi wa Njoro, huku wengi wakieleza kuwa sasa wanaamini michezo inaweza kuwa njia halali ya kujikwamua kimaisha, hasa kwa vijana waliokuwa wakihangaika kuonesha vipaji vyao bila jukwaa la kuviendeleza.

Akizungumza mmoa wa wakazi wa Kata ya Njoro Emanuel Milazo, amepongeza juhudi za kuboresha uwanja huo wa Railway ambao hapo awali ulikuwa na changamoto ya vumbi na hali duni ya miundombinu.

Milazo, ambaye ni mmoja wa waendesha bodaboda eneo hilo, amesema kuwa hali hiyo ilisababisha majeraha kwa vijana waliokuwa wakitumia uwanja huo kwa michezo.

“Tulimfuata Mstahiki Meya na kumweleza hali ya uwanja, alitusikiliza na sasa tunaona matunda ya mazungumzo yale, kama unavyoona uwanja unatengenezwa,” alisema Milazo.

Aidha alisema kuwa kupitia mashindano ya Zuber Cup, Mstahiki Meya Kidumo, ametuahidi kuendelea kuuboresha uwanja huo kwa kuweka jukwaa maalum la viongozi, pamoja na kuvutia wawekezaji zaidi.

Alisema mashindano hayo pia yamekuwa fursa kwa akina mama wajasiriamali, wanaofanya biashara ndogondogo wakati wa michezo, ikiwemo uuzaji wa chakula, vinywaji na mavazi ya michezo.

“Akina mama wanaomba mashindano haya yaanze hata leo kwa sababu fursa ni nyingi sana,” aliongeza.

Gadson Said, mkazi mwingine wa Majengo, alieleza furaha yake kwa maboresho hayo ya uwanja na kutoa pongezi kwa Meya wa Manispaa ya Moshi, Mhandisi Zuberi Kidumo.

“Viwanja bora vinaweza kuleta fursa za biashara na kuongeza mapato ya halmashauri kupitia kodi na matumizi ya viwanja kwa shughuli mbalimbali,” alisema.

Hatua hii inaonyesha jinsi ushirikiano kati ya wananchi na viongozi wa serikali za mitaa unavyoweza kuleta maendeleo chanya na kuboresha maisha ya jamii.

Kwa sasa, tayari timu mbalimbali za vijana zinatarajia kutumia uwanja huo kwa mazoezi na mashindano, huku kukiwa na matarajio makubwa ya kuwapo kwa mashindano ya wilaya na mkoa yatakayosaidia kuibua vipaji zaidi.

Ujenzi wa uwanja huu unatajwa kuwa mfano bora wa namna viongozi wa ngazi za chini wanaweza kuchangia maendeleo ya michezo nchini kupitia uwekezaji katika miundombinu.















Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.