NJORO-MOSHI.
Viongozi wa vyama vya michezo mkoani Kilimanjaro wamepongeza jitihada kubwa zilizofanywa na Diwani wa Kata ya Njoro na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, kwa uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa uwanja wa kisasa wa Railway uliopo Kata ya Njoro.
Wakizungumza jana walipotembelea uwanja huo kwa ajili ya kukagua maendeleo ya miundombinu hiyo, viongozi hao walionesha kufurahishwa na kiwango cha maboresho yaliyofanyika na kuitaja hatua hiyo kuwa ni mkombozi kwa vijana wenye vipaji vya michezo katika Manispaa ya Moshi na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla.
"Nimpongeze sana Mstahiki Meya kwa kazi hii kubwa, uwekezaji huu ni mfano bora wa kuigwa na viongozi wengine, bado tunakabiliwa na uhaba mkubwa wa viwanja vya michezo katika mkoa wetu, lakini kama kila kata ingekuwa na uwanja kama huu, tungekuwa na vipaji vingi sana."Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro, Nelson Mrashan, alisema:
Mrashan alisisitiza kuwa uwekezaji katika viwanja vya michezo ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya michezo, na alitoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza kuwekeza kama alivyofanya Zuberi Kidumo.
"Vipaji vipo mtaani, lakini mazingira ndiyo changamoto, uwanja huu umeweka msingi wa mustakabali mzuri wa michezo kwa vijana wetu," aliongeza.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kilimanjaro (KRFA), Abdallah Thabiti, alimpongeza Mstahiki Meya kwa kushirikiana vyema na wadau wa kata hiyo kuhakikisha uboreshaji wa uwanja unafanyika kwa kiwango bora.
"Tunafahamu uwanja huu ulivyokuwa hapo awali, sasa umebadilika kabisa, tunaleta pongezi zetu kwa Diwani Zueberi Abdallah Kidumo na timu yake, ni wakati sasa kwa wadau wengine kuiga mfano huu ili tuijenge miundombinu ya michezo kwa ajili ya vizazi vijavyo," alisema Thabiti.
Aidha, Japhet Mpande, Mwenyekiti wa Zuberi Cup na Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Manispaa ya Moshi, alibainisha kuwa uwanja huo tayari umezaa matunda tangu kuanza kutumika mwaka 2021.
"Kupitia Zuberi Cup, vijana wengi wameibuka kutoka hapa, wapo walioko kwenye timu za ligi kuu kama vile Ken Gold, JKT Ruvu, hadi Waydadi, huyu kijana Seleman Mwalimu ni mfano wa mafanikio yanayotokana na uwanja huu wa Railway Njoro," alisema.
Mpande aliongeza kuwa mashindano ya Zuberi Cup Tournament yamekuwa chachu ya maendeleo ya vipaji, huku akitangaza kuwa bonanza maalum la maandalizi ya msimu 2025 litaanza Juni 13, 2025 ambapo mashindano hayo yatafanyika katika uwanja wa Majengo ambao pia umeboreshwa chini ya usimamizi wa Meya Kidumo.
"Zuberi hakuwa tu kiongozi; alikuwa mchezaji mwenyewe, alikuwa nahodha wa timu ya Eagle na pia timu ya Shule ya Ufundi Moshi, hivyo anaelewa thamani ya michezo na sasa anaionyesha kwa vitendo," alisema Mwl. Mpande.
Viongozi hao wamesisitiza kuwa maendeleo ya michezo hayawezi kufikiwa bila uwepo wa viwanja bora, huku wakiwataka viongozi wa halmashauri, wadau wa sekta binafsi na mashirika mbalimbali kushirikiana katika kuwekeza kwenye miundombinu ya michezo kama njia ya kuwawezesha vijana kupata ajira, kuibua vipaji na kujenga taifa lenye afya.








