MOSHI.
Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi (FITI) kimepata kibali maalum cha kudahili wanafunzi watakaonufaika na mikopo ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kwa asilimia 100, ikiwa ni hatua kubwa ya kuwawezesha vijana wengi kupata elimu ya vitendo na ujuzi wa uhifadhi na matumizi ya rasilimali za misitu nchini.
Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Lupala Zacharia, alisema hayo Juni 10,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisni kwake ambapo alisema kwa mwaka wa fedha 2025/2026 chuo cha Viwanda Vya Misitu Moshi (FITI) kimekuwa ni miongoni mwa vyuo vilivyochaguliwa kudahili wanafunzi watakaojiunga na Astashahada ya Teknolojia ya Viwanda vya Misitu.
"Tangu kuanzishwa kwa chuo hiki mwaka 1976 hakijawahi kupata mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na serikali, kwa mwaka huu tumepata kibali cha kudahili wanafunzi watakaonufaika na mikopo hiyo,"alisema Dkt. Zacharia.
Alisema kwa sasa wanafunzi wanaodahiliwa kwenye programu ya Astashahada wanapata mkopo kwa asilimia 100, hatua hii ni ya kihistoria kwa chuo chetu cha FITI, kwani hapo awali haikuwa kawaida kwa wanafunzi wetu kupata mikopo ya serikali.
Aliongeza kuwa tayari kuna Afisa maalum wa mikopo aliyeteuliwa na chuo hicho ili kuwasaidia wanafunzi katika taratibu zote za upatikanaji wa mikopo.
Aidha, alisema wanafunzi waliokuwa wakiendelea na masomo yao chuoni hapo wameanza kunufaika na mikopo hiyo, ambapo asilimia 50 yao tayari wamepata mikopo kupitia HESLB.


