FITI YAHUISHA MITAALA YA NACTVET KUKIDHI MAHITAJI YA SOKO LA AJIRA NA TEKNOLOJIA

  
                                                            
                                                 MOSHI-KILIMANJARO

Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limeanza mchakato wa uhuishaji wa mitaala ya Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi (FITI), kwa lengo la kuhakikisha inalingana na mahitaji ya sasa ya soko la ajira, maendeleo ya teknolojia na mabadiliko ya sekta ya misitu nchini.


Hayo yamebainishwa Juni 10,2025 na Afisa Mdhibiti Ubora Mkuu wa Mitaala kutoka NACTVET, Dkt. Edward Joseph Mneda, wakati wa ufunguzi wa Warsha ya kupitia mitaala ya chuo hicho kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo alisema mitaala hiyo ilikuwa ikitumika kwa zaidi ya miaka mitano, na sasa inapitiwa upya ili kuendana na mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kitaaluma.

Alisema mitaala wanayohuisha  inalenga kutoa mafunzo ya vitendo zaidi ili kuhakikisha kijana anayehitimu kutoka FITI ana uwezo wa kujiajiri, si kusubiri ajira na kwamba kupitia mapitio hayo yanahusisha wadau mbalimbali wa sekta ya misitu, mazingira na viwanda.


Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha FITI, Dkt. Lupala Zacharia, alisema chuo hicho sasa kimepata kibali maalum cha kudahili wanafunzi watakaonufaika na mikopo ya asilimia 100 kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), hasa kwa wale wanaojiunga na Astashahada ya Teknolojia ya Viwanda vya Misitu.

Alisema tayari chuo kimeweka afisa maalum wa mikopo kusaidia wanafunzi kukamilisha taratibu husika, ambapo kwa sasa asilimia 50 ya wanafunzi walioko chuoni hapo tayari wameanza kupokea mikopo kupitia HESLB.

Aidha alisema chuo hicho. kimepewa kibali cha kuendesha mafunzo ya ufundi kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), yakiwemo masomo ya useremala, ufundi wa misitu, na uchakataji wa mazao ya misitu.
 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Edward Kohi, alisisitiza kuwa mchakato wa kuhuisha mitaala na uwekezaji katika FITI ni sehemu ya mkakati wa taifa wa kuwaandaa vijana wenye ujuzi wa kisasa katika bidhaa za misitu zilizohandisiwa.


Katika hatua nyingine mkuu huyo wa chuo alitoa wito kwa vijana wa Kitanzania kuchangamkia fursa zinazopatikana chuoni hapo, akieleza kuwa FITI ni kitovu cha elimu ya amali inayojikita katika ujuzi, ubunifu, na ajira kwa vijana wa sasa na baadaye.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.