MNZAVA AFUNGUA MAFUNZO YA JESHI LA AKIBA, AWAPONGEZA MADIWANI KUJIUNGA KWA HIARI

MOSHI-KILIMANJARO.

MKUU wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, amefungua mafunzo ya Jeshi la Akiba Manispaa ya Moshi, huku akiwapongeza madiwani nane wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa kuamua kwa hiari kujiunga na mafunzo hayo, akieleza kuwa hatua hiyo ni ishara ya uzalendo na utayari wa kulitumikia taifa.

Akizungumza katika Uwanja wa Mashujaa, Manispaa ya Moshi, wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mnzava alisema kundi la washiriki linajumuisha vijana kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, wakiwemo madiwani na viongozi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.

Alisema uamuzi wa viongozi hao kushiriki mafunzo ya Jeshi la Akiba unaonesha mfano bora wa uongozi unaotanguliza maslahi ya taifa na kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za ulinzi na usalama wa nchi.


"Jeshi la Akiba lina mchango mkubwa katika kuimarisha ulinzi na usalama wa taifa. Askari wake wamekuwa msaada muhimu wakati wa matukio mbalimbali ya kitaifa, hivyo tunapaswa kuendelea kulipa kipaumbele. Kundi hili litakapohitimu mafunzo litaongeza nguvu kazi ya askari wa akiba tulionao," alisema Mnzava.

Aliwataka washiriki wote kuzingatia nidhamu, utulivu na kufuata maelekezo ya wakufunzi wao ili waweze kuhitimu mafunzo hayo kwa mafanikio na kuwa raia wenye uzalendo na utayari wa kulitumikia taifa wakati wowote watakapohitajika.

Kwa upande wake, Kaimu Mshauri wa Jeshi la Akiba Wilaya ya Moshi, Richard Kapiki, alisema mafunzo hayo yatawajengea washiriki uwezo wa kiulinzi na kuwaandaa kushiriki kikamilifu katika shughuli za ulinzi na usalama wa taifa.

Alisema washiriki watapatiwa mafunzo ya ukakamavu, mbinu za kivita, uraia, matumizi ya silaha, huduma ya kwanza, usomaji wa ramani, sheria za kijeshi, uwanja wa porini (field craft), pamoja na mazoezi ya utimamu wa mwili.

Kapiki alisema mafunzo hayo yataendeshwa kwa ushirikiano wa taasisi mbalimbali za ulinzi na usalama, zikiwemo Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Jeshi la Magereza, Idara ya Uhamiaji, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Usalama wa Taifa pamoja na wakufunzi wa ujasiriamali.

Alieleza kuwa mafunzo hayo ya awali yatachukua jumla ya wiki 16, yakifanyika kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa, huku kila wiki ikiwa na vipindi vitano vya dakika 40 kila kimoja.

Aidha, alisema mafunzo hayo yanafanyika katika Uwanja wa Mashujaa uliopo Kata ya Kiusa pamoja na eneo la Mikameni, Kata ya Kahe.

Kapiki alibainisha kuwa mafunzo hayo ni wazi kwa Watanzania wote wenye uzalendo bila kujali jinsia, dini wala itikadi za kisiasa, mradi wawe na umri unaokubalika kisheria, afya njema na watimize masharti yaliyowekwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za Jeshi la Akiba.


Naye Diwani wa Kata ya Njoro na Meya wa Manispaa hiyo Mhandisi Zuberi Abdallah, amesema wameamua kujiunga na Jeshi la Akiba, kwa hiari ili kuhamasisha jamii hususan vijana kushiriki katika shughuli za Ulinzi na Usalama.

"Kitu bora ni ile akiba, akiba unayojiwekea nyumbani kwako au benki, inakuwa bora kuliko ile unayokuwq nayo mfukoni, unaposikia Jeshi la Akiba ni bora sana, sisi madiwani tumeamua kujiunga na Jeshi la Akiba kwa hiari ili kuonesha uzalendo, miili yetu iwe vizuri, kuhamasisha amani kwa nchi yetu."alisema Kidumo.

Jumla ya washiriki 123 wameandikishwa katika kundi hilo, wakiwemo wanawake 42 na wanaume 81.





























Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.