SERIKALI KUTOA FEDHA KWAAJILI YA UJENZI WA KITUO CHA AFYA KIBOROLONI

                                                               DODOMA

Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange, amesema Serikali imeshatenga Shilingi bilioni 53.5 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya kimkakati katika majimbo mbalimbali, ambapo Shilingi bilioni 30 tayari zimeshatolewa na ziko kwenye halmashauri husika.

Dkt. Dugange alitoa kauli hiyo Juni 16,2025 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Priscus Tarimo, ambaye alitaka kufahamu lini fedha zitatolewa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kiboroloni, kilichoteuliwa kuwa kituo cha kimkakati kwa wananchi wa eneo hilo.

Katika swali lake, Mbunge Tarimo alisema: “Zahanati ya Kiboroloni ndiyo tuliyoichagua kama kituo cha afya cha kimkakati. Je, ni lini fedha zitapelekwa kwa ajili ya kituo hicho?”

Akijibu swali hilo, Dkt. Dugange alimtoa wasiwasi mbunge huyo na wananchi wa Moshi Mjini kwa kusema: “Nikuhakikishie Mbunge Tarimo kwamba tutahakikisha tunapeleka fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kiboroloni, ili kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi wa eneo hilo.”

Dkt. Dugange alisisitiza kuwa serikali inaendelea na mkakati wa kuimarisha huduma za afya katika maeneo mbalimbali nchini kupitia miradi ya kimkakati, ikiwa ni pamoja na kujenga na kuboresha vituo vya afya katika maeneo yenye mahitaji makubwa ya huduma hizo.

Kwa mujibu wa taarifa ya TAMISEMI, utekelezaji wa miradi hiyo unalenga kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.