SERIKALI YATOA UFAFANUZI KUHUSU MAKATO KATIKA MALIPO YA WASTAAFU

                                     BUNGENI-DODOMA.

Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeeleza sababu za makato yanayofanyika katika mafao ya wastaafu, kufuatia swali la Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Jacob Tarimo, aliyetaka kufahamu ni kwa nini serikali inafanya makato katika malipo ya wastaafu, na iwapo makato hayo ni ya kodi.

Akijibu swali hilo bungeni kwa niaba ya Waziri Mkuu, Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi, alisema kuwa sheria zinazosimamia mifuko ya hifadhi ya jamii haziruhusu makato yoyote ya kodi katika mafao ya wastaafu.

Aidha Naibu Waziri Katambi alisema “Pale inapobainika kuwa mstaafu ana deni kutoka serikalini ambalo halijalipwa hadi muda wa kustaafu, sehemu ya mafao yake hukatwa kwa ajili ya kufidia deni hilo.”

Baada ya majibu hayo, Mbunge  Tarimo aliuliza maswali mawili ya nyongeza, akitaka kujua iwapo Serikali iko tayari kufuatilia malalamiko ya wastaafu kuhusu makato yasiyoeleweka, na pia iwapo Serikali iko tayari kufanya marekebisho kwa wastaafu waliokuwa wakipokea mishahara midogo ili nao wapate pensheni inayolingana na hali ya sasa.

Akijibu, maswali mawili ya nyongeza Naibu Waziri Katambi;  alimhakikishia Mbunge huyo kuwa Serikali iko makini katika kuhakikisha haki za wastaafu zinalindwa, na tayari imefanya maboresho ya kisheria katika mifuko ya PSSSF na NSSF ili kuzuia matumizi yoyote ya pensheni kinyume na kusudio lake halali.

“Makato yoyote yasiyoeleweka ni marufuku kisheria,” alisisitiza Naibu Waziri Katambi. “Isipokuwa tu kama ni deni lililo halali kwa mujibu wa sheria, hata makubaliano nje ya utaratibu wa mifuko hayawezi kuruhusiwa.”

Aidha, alieleza kuwa serikali inaendelea kufanya mapitio ya mfumo wa pensheni ili kuhakikisha haki na usawa kwa wastaafu wote, ikiwemo suala la kutazama upya viwango vya pensheni kwa wastaafu wa zamani waliokuwa na mishahara midogo.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.