MBUNGE NDAKIDEMI AHOJI SERIKALI KUHUSU RUZUKU YA VIUATILIFU KWA WAKULIMA WA ZAO LA KAHAWA

                                             

                                             DODOMA.

Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi, Juni 16, 2025 alihoji bungeni mpango wa serikali wa kuwapatia wakulima wa kahawa viuatilifu bure au kwa bei nafuu, kutokana na changamoto kubwa ya wadudu waharibifu wanaoshambulia zao hilo.

Katika swali lake la nyongeza, Profesa Ndakidemi alisema kuwa licha ya wakulima hao kunufaika na miche ya kahawa iliyotolewa na serikali, bado wanakabiliwa na uharibifu mkubwa unaotishia tija na ubora wa zao hilo la kimkakati.

“Tunaishukuru sana serikali kwa kuwapatia wakulima wa Jimbo la Moshi Vijijini miche ya kahawa. Je, serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia wakulima hawa wapate viuatilifu bure au kwa bei ya ruzuku?” aliuliza Profesa Ndakidemi.

Akijibu, Naibu Waziri wa Kilimo, David  Silinde, alisema serikali inalifahamu suala hilo na kwamba iko kwenye hatua za utekelezaji wa mpango wa upatikanaji wa viuatilifu kwa mazao ya kimkakati ikiwemo zao la kahawa.

“Kwanza napenda kumpongeza Profesa Ndakidemi kwa kazi nzuri anayofanya katika Jimbo la Moshi Vijijini na kwa kufuatilia zao la kahawa, nami nilishiriki naye kugawa bure miche ya kahawa kwa mfumo wa ruzuku,” alisema Naibu Waziri Silinde.

Alisema “Mpango wa sasa ni kuhakikisha tunawawezesha wakulima kupunguza gharama za uzalishaji, tumeanza na korosho, tutakwenda kwenye kahawa na mazao mengine, zao la kahawa tayari liko kwenye mipango ya serikali,” aliongeza.

Zao la kahawa ni miongoni mwa mazao yanayoingiza fedha za kigeni na kuchangia ajira kwa maelfu ya wakulima nchini, hasa katika mikoa ya Kaskazini kama Kilimanjaro, Arusha na Kagera.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.