MOSHI-KILIMANJARO.
Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi (FITI) kimeanzisha kozi fupi ya biashara ya hewa kaboni ili kuhakikisha Watanzania wananufaika na fursa mpya ya kiuchumi kupitia utunzaji wa mazingira na misitu.
Akizungumza jana na Waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Lupala Zakaria, alisema Tanzania ina utajiri mkubwa wa misitu unaofikia asilimia 55 ya ardhi yote, lakini bado wananchi wengi hawana ujuzi wa kunufaika na biashara ya hewa kaboni inayokua kwa kasi duniani.
“Chuo chetu kina kaulimbiu isemayo ‘Misitu ni Fedha na Ajira’. Ndani ya misitu ambayo nchi yetu imebarikiwa kuwa nayo, kuna utajiri mkubwa ambao kama vijana wataelimika vizuri, unaweza kuwatoa kwenye umasikini,” alisema Dkt. Zakaria.
Alieleza kuwa pamoja na Tanzania kuwa na kiwango kikubwa cha hewa kaboni, changamoto iliyopo ni ukosefu wa ujuzi juu ya namna ya kuingia kwenye biashara hiyo. hivyo, kozi hiyo mpya imelenga kuwajengea uwezo vijana na makampuni nchini ili kushiriki kikamilifu katika masoko ya kimataifa ya kaboni.
“Tunataka kampuni zenye uwezo wa kuzalisha wataalamu wa biashara ya hewa kaboni, ikiwemo kuandaa mawazo ya biashara, upimaji wa kaboni, na majadiliano ya biashara katika soko la kimataifa,” aliongeza.
Aidha, Dkt. Zakaria alisema FITI ina wataalamu waliobobea katika sekta hiyo, ambao wako tayari kusaidia Watanzania kuanzisha makampuni ya uwakala wa biashara ya kaboni (carbon blockers) na kusaidia kulinda mazingira kupitia biashara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Edward Kohi, aliipongeza FITI kwa kuendelea kutoa mafunzo ya vitendo yenye kuendana na mahitaji ya sasa ya soko la ajira.
“Tunataka kuona vijana wetu wanakuwa wabobezi katika bidhaa za mbao zenye viwango vya kimataifa, hili litaongeza ajira, kuchochea uchumi wa viwanda na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje,” alisema Dkt. Kohi.
Naye Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Kanda ya Kaskazini, James Nshare, alitoa wito kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuwahamasisha vijana kutumia fursa zinazotolewa na Chuo cha FITI ili waweze kujiajiri na kujipatia kipato.
“Chuo hiki kina fursa nyingi, vijana wakizitumia vizuri wataweza kupata ajira, kipato na hata kuchangia pato la taifa kupitia fedha za kigeni,” alisema Nshare.
Biashara ya hewa kaboni ni mfumo wa kulipia huduma ya uhifadhi wa mazingira kwa kupunguza utoaji wa gesi chafu, ambapo maeneo ya misitu yanatumika kama "sink" ya kunyonya kaboni.
Tanzania, ikiwa na rasilimali nyingi za misitu, ina nafasi kubwa ya kunufaika kupitia mfumo huo ikiwa ujuzi utatolewa kwa wakati.









