URU-KUSINI
Wananchi wa Kata ya Uru Kusini, Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, wameonesha imani na upendo wao kwa aliyekuwa Diwani wao, Wakili Wilhad Kitaly, kwa kumchangia kiasi cha Shilingi 226,000 ili kumwezesha kuchukua fomu ya kugombea tena nafasi ya Udiwani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika ukumbi wa Chama cha Msingi Uru-Kati, wananchi hao walieleza kuwa wameona sababu za msingi za kumrejesha tena uongozini kutokana na utendaji wake mahiri, usiochoka na wenye matokeo chanya kwa maendeleo ya Kata yao.
Miongoni mwa mafanikio makubwa waliyoyataja ni pamoja na kutatuliwa kwa changamoto sugu ya upatikanaji wa maji safi na salama, ambayo kwa miaka mingi ilikuwa kero kwa wananchi wa Uru Kusini, kupitia juhudi za Diwani Kitaly, sasa wakazi hao wanapata huduma ya maji majumbani mwao kwa uhakika.
Aidha, wananchi walieleza kuwa kabla ya uongozi wake, wengi wao hawakuwa na hati miliki za viwanja, hali iliyochochea migogoro ya ardhi kwa kiwango kikubwa, Diwani Kitaly alisimama kidete kuhakikisha wananchi wake wanapata hati halali, hatua ambayo imeimarisha usalama wa umiliki wa ardhi na kuondoa migogoro iliyokuwepo.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020–2025, Wakili Wilhad Kitaly alieleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wake wa miaka mitano, ikiwemo:
Sekta ya miundombinu: Ukarabati wa barabara na vivuko, pamoja na mifereji ya asili. kwenye upande wa Elimu: Ukamilishaji wa bwalo la chakula kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mawella, ukarabati wa shule chakavu, ujenzi na uboreshaji wa vyoo mashuleni.
Katika Sekta ya afya: Ujenzi wa Kituo cha Afya Uru Kusini, jengo la kliniki, nyumba za watumishi, jengo la kujifungulia, jengo la upasuaji, na ujenzi wa hospitali ya Mawella.
Kwenye Sekta ya Kilimo na uchumi: Diwani Kitaly alisema alifanikisha Uhamasishaji wa kilimo cha mboga mboga na ufugaji wa kisasa, huku eneo la Utawala: alifanikisha Ujenzi wa ofisi za Vijiji na ofisi ya Kata.
Katika eneo la Mazingira na michezo: alisema alifanikisha kuimarisha usafi wa mazingira, kuhifadhi vyanzo vya maji, na kuendeleza mashindano ya michezo.
Wakili Kitaly alitumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wa Uru Kusini kwa ushirikiano waliompa katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake, huku akitangaza rasmi nia ya kugombea tena nafasi ya Udiwani mwaka 2025, ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.
Wananchi wametoa kauli moja: "Hatuna cha kumpa zaidi ya kumuunga mkono kwa vitendo." Na kwa hilo, wameonyesha wazi kuwa sauti ya wananchi ndiyo sauti ya Mungu.

















