MOSHI-KILIMANJARO.
Umoja wa Vikundi Marangu (UVIMA SACCOS LTD) umeadhimisha miaka 18 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007, ikiwa ni kipindi ambacho kimeweka rekodi ya utoaji wa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 6.4 kwa wanachama wake.
Akizungumza katika mahojiano maalumu, Meneja wa UVIMA SACCOS, Jackson Amani Mtui, alisema taasisi hiyo imepiga hatua kubwa za kimaendeleo tangu kuanzishwa kwake, ikijijengea uwezo wa kujitegemea kifedha bila kutegemea mikopo ya nje.
“Tulianza na mtaji wa shilingi milioni 6, lakini leo hii tunajivunia kuwa na mtaji wa zaidi ya shilingi milioni 234 uliotokana na juhudi za wanachama na uongozi makini,” alisema Mtui.
Alisema kuwa SACCOS hiyo ilianza na hisa zenye thamani ya shilingi milioni 7, na hadi sasa zimeongezeka hadi kufikia zaidi ya shilingi milioni 169, huku mali za taasisi zikifikia thamani ya shilingi milioni 830.
Kwa sasa, UVIMA SACCOS inahudumia wanachama takriban 1003, ikiwa na mtaji jumla wa shilingi 238,908,731, unaojumuisha hisa, akiba mbalimbali za kisheria, malimbikizo ya faida na misaada ya mali.
"Katika kipindi hicho cha miaka 18, UVIMA SACCOS imefanikiwa, kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 4.6, kujijengea mtaji wa ndani bila kutegemea mikopo ya nje, kuimarisha matumizi ya TEHAMA kwa kuanzisha tovuti rasmi, kutoa elimu ya ujasiriamali na mafunzo ya kilimo hai kwa wanachama."
Mtui aliongeza kuwa malengo ya baadaye ni kuifanya UVIMA SACCOS kuwa taasisi imara ya kifedha inayotoa huduma bora, kuimarisha maisha ya jamii ya kipato cha chini hususan vijijini.
"Tunataka kuendelea kutoa elimu ya ushirika na ujasiriamali ili wananchi waweze kutumia fursa za kiuchumi na kujikomboa na umasikini," alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVIMA SACCOS LTD, Mungubariki Joram Tarimo, amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa SACCOS hiyo mwaka 2007, kumekuwa na mafanikio ambayo wanachama wanajivunia, ikiwemo kujikwamua kiuchumi kupitia mikopo ya elimu, kilimo, ufugaji na ujenzi wa makazi.
Alisema pia kwamba UVIMA SACCOS imekuwa ikipata hati safi kwa kipindi cha miaka 15 mfululizo, jambo linaloonyesha uwazi na uwajibikaji katika uendeshaji wake.
Mwanzilishi wa SACCOS hiyo, ambaye pia ni Mkurugenzi Mstaafu wa Floresta Tanzania, Edith Banzi, alionesha furaha yake kuona taasisi aliyoianzisha ikiendelea kufanya kazi kwa ufanisi na kuwanufaisha wanachama.
Baadhi ya wanufaika wa UVIMA SACCOS wameshukuru kupata mikopo iliyowawezesha kununua vifaa vya biashara, kusomesha watoto wao, kujenga nyumba na kununua mifugo.








