MIKOA 16 YAWANIA TAJI LA KAHAWA BORA

MBEYA-TANZANIA.

Zaidi ya sampuli 70 za kahawa zinazolimwa katika mikoa 16 nchini zimekusanywa Jijini Mbeya kwa ajili ya kushindanishwa ili kupata kahawa moja bora itakayowakilisha Tanzania kwenye mashindano ya ubora wa kahawa katika soko la Afrika.

Shindano hilo limeandaliwa na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kwa kushirikiana na wadau wa zao hilo, likiwa na lengo la kutafuta kahawa bora zaidi nchini ambayo itaongeza ushindani wa Tanzania katika masoko ya kimataifa.

Mashindano hayo yamehusisha kahawa kutoka mikoa ya Mbeya, Kilimanjaro, Songwe, Katavi, Kagera, Mara, Njombe, Ruvuma na Kigoma, mikoa mingine inayoshiriki ni Geita, Mwanza, Tanga, Iringa, Manyara, Morogoro, Arusha na Rukwa, ambako huzalishwa kahawa aina ya Arabika na Robusta.

Mkurugenzi wa Ubora wa Kahawa kutoka TCB, Frank Nyarusi, alisema sampuli hizo zimeonwa na kupigiwa kura na wadau, na ile itakayopata kura nyingi ndiyo itawasilishwa kwenye masoko ya kimataifa kwa ajili ya mashindano ya ubora wa kahawa.

Alieleza kuwa mashindano hayo ni moja ya mbinu za Bodi ya Kahawa na wadau katika kuhamasisha wakulima kuongeza ubora wa kahawa nchini, hivyo kuongeza thamani na fedha za kigeni nchini.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazozalisha kahawa barani Afrika, kwa sasa tupo hapa kwa siku 14 kuchagua kahawa bora zaidi itakayoshindanishwa kimataifa,” alisema Nyarusi.

Alifafanua kuwa mashindano hayo yanahusisha aina tano za kahawa zinazozalishwa kwa kiwango kikubwa nchini: Arabika, Robusta, Arabika laini, Arabika ngumu na kahawa ya ubunifu.

Kwa mujibu wa Nyarusi, majaji saba kutoka ndani na nje ya nchi wameteuliwa kuonja na kutoa alama kwa kila sampuli. Majaji hao ni miongoni mwa wataalamu wa juu wa tathmini ya ladha na ubora wa kahawa.

Mmoja wa majaji hao, Bala Mlinyula, alisema kahawa hizo hupangwa katika makundi matatu,bora zaidi, bora wastani na kawaida.

Alibainisha kuwa kazi yao ni kuonja na kupima kila sampuli bila kufahamu ilikotoka, ili kuepusha upendeleo wowote.

“Wakati wa kuonja hatujui kahawa imetoka mkoa gani au mkulima gani. Tunapanga kwa madaraja kulingana na ubora, kahawa bora zaidi hutakiwa kufikia asilimia 100,” alisema Mlinyula.

Mlinyula aliongeza kuwa taarifa wanazojaza kwenye fomu maalumu ndizo zitakazosaidia kutambua sampuli itakayoshinda na baadaye kuiwakilisha Tanzania kwenye soko la kimataifa.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa mashindano hayo, Philip Athlack kutoka Poland, alisema wanatumia vigezo vya kimataifa katika upangaji wa madaraja ya kahawa ili kuhakikisha ushindani unazingatia viwango vinavyotakiwa duniani.

Alisema kutumia vigezo vya kimataifa si tu kunawawezesha kupata kahawa bora, bali pia kunasaidia wakulima kufahamu maeneo ya kuboresha uzalishaji ili kufikia viwango vinavyohitajika na soko la dunia.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.