MOSHI-KILIMANJARO.
MAZINGIRA ya kisiasa ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi yamepata sura mpya baada ya mwandishi wa habari wa Radio Sauti ya Injili, Samuel Ndetaramo Shao, kutangaza rasmi kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hatua hiyo imeibua mjadala mpana kuhusu nafasi ya Wataalamu wa Mawasiliano katika uongozi wa serikali za mitaa, pamoja na mwelekeo mpya wa maendeleo unaoweza kuletwa na kizazi kipya cha viongozi wenye weledi na shauku ya kutumikia wananchi.
Shao alichukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama Novemba 20, mwaka huu, hatua aliyosema imekuja baada ya kujitathmini na kubaini kuwa ana uzoefu, uelewa na nia njema ya kuongoza.
Anaeleza kuwa uamuzi wake sio tu wa kutafuta nafasi ya uongozi, bali ni dhamira ya dhati ya kuimarisha ushirikiano kati ya madiwani na uongozi wa Halmashauri, ili kuhakikisha utekelezaji wa majukumu unakwenda kwa kasi na kwa manufaa ya wananchi wa Moshi vijijini.
Shao ni mhitimu wa Chuo cha Uandishi wa Habari cha Royal College of Journalism, na pia anashikilia Diploma ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (IJMC) aliyoipata jijini Dar es Salaam.
Taaluma yake imempa uwezo wa kuchambua masuala ya kijamii na kiutawala, kusikiliza wananchi, na kufuatilia kwa undani changamoto zinazowakabili.
Katika mahojiano, Shao anasisitiza kuwa uandishi wa habari umemjenga kuwa kiongozi mwenye uwezo wa kuelewa kwa upana masuala ya wananchi na kuyatolea suluhisho.
“Taaluma yangu imenipa nafasi ya kuwa karibu na jamii, kuona changamoto zao kwa macho yangu, na kusikia kilio chao, hii imenifanya nitamani kutumikia zaidi kwenye ngazi ya utawala wa halmashauri,” anasema.
Mbali na taaluma ya uandishi wa habari, Shao amehudumu kama Diwani wa Kata ya Mwika Kaskazini, na anasema nafasi hiyo imemfundisha mengi kuhusu utendaji wa serikali na changamoto za kusimamia maendeleo.
Anasema ametumia muda wake mwingi kujifunza mwenendo wa Halmashauri, vyanzo vya mapato, changamoto za kibajeti na namna ya kutatua migogoro ya wananchi.
“Nimejifunza mengi nikiwa diwani, nimeona namna mambo yanavyokwenda, changamoto za utendaji na umuhimu wa kuwa na viongozi wasio na uoga wa kusema na kutenda, nimepima na kuona kuwa sasa nina uzoefu wa kutosha,” Shao anaeleza kwa kujiamini.
Anafafanua kuwa Halmashauri ya Moshi ina fursa nyingi za maendeleo, lakini changamoto kubwa imekuwa ukosefu wa ushirikiano baina ya baadhi ya madiwani na watendaji, pamoja na vikwazo vya mapato.
"Ni wakati wa kuwa na Makamu Mwenyekiti anayeweza kuwaunganisha wote na kuhakikisha maslahi ya wananchi yanawekwa mbele,” anasema.
Shao anabeba ajenda kadhaa za kimkakati ambazo ameahidi kuzitekeleza endapo atapata ridhaa ya kuongoza kama Makamu Mwenyekiti.
Kwa upande wa utawala bora, anasema atawekeza katika kuimarisha mawasiliano na uwazi kati ya uongozi wa Halmashauri na madiwani.
"Nitawezesha madiwani kupata taarifa sahihi kwa wakati, kusikilizwa na kuheshimiwa, madiwani wakifanya kazi bila vikwazo, maendeleo yataenda kwa kasi,” anasisitiza.
Kwenye masuala ya mapato, Shao ameahidi kuziba mianya ya upotevu wa fedha za umma na kubuni vyanzo vipya vya mapato kwa manufaa ya wilaya.
Anasema mapato ya ndani yakisimamiwa vizuri yataongeza uwekezaji kwenye sekta za afya, elimu, maji na kilimo.
Katika upande wa makundi maalum, hasa watu wenye ulemavu, Shao amesema amekuwa akishuhudia kwa muda mrefu ukosefu wa haki na huduma kwa kundi hilo, hivyo atahakikisha wanapata nafasi sawa kama wananchi wengine.
“Nitahakikisha haki ya mtu mwenye ulemavu inalindwa, wamekuwa wakinyimwa fursa nyingi kutokana na ulemavu wao hilo sitalikubali,” anasema kwa msisitizo.
Shao, anafafanua kuwa, anaamini vijana ni nguvu muhimu katika ujenzi wa uchumi ndani ya wilaya, ameahidi kuhamasisha vijana kuunda vikundi vya uzalishaji mali ili waweze kunufaika na mikopo inayotolewa na halmashauri.
“Tunapaswa kuwafanya vijana wajitegemee kwa kuanzisha miradi ya kilimo, ufugaji na ujasiriamali, halmashauri ina fedha, lakini vijana wetu hawafikiwi kikamilifu. Nitahakikisha mnufaiko unaongezeka,” anasema.
Katika sekta ya miundombinu, Shao ameweka wazi kuwa kipaumbele chake kitakuwa kuhakikisha barabara zote muhimu zinapitika mwaka mzima.
Anasema barabara nyingi za vijijini zimekuwa zikiharibika mara kwa mara kutokana na mvua, jambo linalokwamisha shughuli za kiuchumi na kijamii.
Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi, Ramadhani Mahanyu, amesema mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu ulianza Novemba 20 na kukamilika Novemba 21 mwaka huu.
Mahanyu amesisitiza kuwa chama kitaendesha mchakato huo kwa haki na uwazi ili kila mgombea mwenye nia na sifa apate nafasi ya kutimiza ndoto yake.
Anasema nafasi zinazogombewa ni mbili, Mwenyekiti wa Halmashauri na Makamu Mwenyekiti na chama kitahakikisha kinawapata viongozi watakaoleta mageuzi kwa wananchi.
Kwa kujitosa kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Samuel Shao ameleta mwamko mpya wa kisiasa ndani ya Halmashauri ya Moshi.
Kupitia uzoefu wake katika uandishi wa habari na uongozi wa kata, ameonyesha kuwa ana dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko chanya.
Safari yake sasa iko mikononi mwa chama na wanachama watakaopima uwezo, uadilifu na maono yake.







