MKURUGENZI WA KISANGARA TOURS, AWAPONGEZA WANACHAMA WA KIKUNDI CHA UTULIVU FAMILY KUANZISHA KIKUNDI CHA KUSAIDIANA

MWANGA-KILIMANJARO 

Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Kisangara, Frida Mberesero, amewapongeza wanachama wa Kikundi cha Utulivu Family kilichopo Kijiji cha Lang’ata Bora, kwa kuanzisha kikundi cha kusaidiana.

Frida ameyasema jana wakati wa hafla fupi ya uzinduzi rasmi wa kikundi hicho, ambapo aliwachangia wanachama Shilingi laki tano (500,000) na kuwahimiza kuanzisha miradi itakayoongeza kipato na kupunguza mzigo wa michango ya mara kwa mara.

“Maendeleo ni muhimu sana, na hakuna anayeweza kufanikisha jambo peke yake. Niwapongeze kwa kuanzisha kikundi hiki, ila nawasihi muanzishe mradi utakaowaingizia kipato,” alisema Mberesero.

Kwa upande Afisa Mtendaji wa Kata ya Lang’ata, Yakobo Ibrahimu, alivitaka vikundi vya kijamii vilivyopo katika Kata hiyo, kujisajili rasmi serikalini ili kupata uhalali wa kisheria pamoja na kustahili kunufaika na mikopo na fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali.

Aliwasihi wanajamii wanaounda vikundi kuhakikisha wanazingatia utaratibu wa kujisajili, huku akikipongeza Kikundi cha Utulivu Family kwa kutimiza masharti yote yanayotakiwa na Serikali.

Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Lang’ata Bora, Edward Kifalu, aliwataka viongozi wa kikundi kuhakikisha wanaendesha shughuli zao kwa misingi ya uwazi na ukweli ili kudumisha umoja na malengo waliyokusudia.

“Muungano wenu uwe wa kweli, viongozi hakikisheni mnasimama katika misingi ya uwazi na ukweli,” alisema Kifalu.

Awali akitoa taarifa ya kikundi hicho kwa mgeni rasmi, Mwenyekiti wa kikundi, Paulo Mapunda, alisema kikundi kilianzishwa kutokana na gharama kubwa za matibabu na hali ngumu za kiuchumi wanazokutana nazo pale wanapokuwa na wagonjwa.

“Lengo la kuanzisha kikundi chetu ni baada ya kuona gharama kubwa za matibabu na hali yetu ya kiuchumi kutufanya tushindwe kukabiliana na changamoto hizi,” alisema Mapunda.

Mapunda aliongeza kuwa kikundi hutoa mchango wa shilingi laki tano kwa mwanachama anayelazwa hospitalini, na pia huchangia katika shughuli za mazishi.

Akizungumza mmoja wa wanachama wa Utulivu Family, Grace Mmanga, alitoa ushuhuda wa jinsi kikundi hicho kilivyomsaidia kugharamia matibabu yake baada ya kugundulika na uvimbe tumboni uliohitaji upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.

Grace alisema alihitajika kulipia shilingi milioni 1.4, lakini kutokana na changamoto ya kifedha, aliomba msaada kwa kikundi hicho ambacho kilimchangia shilingi laki tano, huku familia yake ikimalizia kiasi kilichokosekana.

"Nilikuwa ninasumbuliwa na uvimbe tumboni na nilitakiwa kulipia shilingi milioni 1.4. Kutokana na hali duni kifedha, kikundi kilinichangia laki tano na familia yangu ikaongeza kiasi kilichokosekana. Ninawashukuru sana kwa kunisaidia kufanikisha gharama za matibabu,” alisema Grace.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.