KIPANDE CHA RELI MOSHI-ARUSHA CHAHUJUMIWA, VIFAA VYA MATARUMA VYANG'OLEWA

BOMAMBUZI

Watu wasiojulikana wameharibu kipande cha reli inayotoka Moshi mkoani Kilimanjaro kuelekea Jijini Arusha kwa kung'oa na kuiba vifungio vya mataruma ya reli, kisha kwenda kuuza kama vyuma chakavu.

Tukio hilo linadaiwa kutokea Aprili 21, 2025 mjira ya saa tano na nusu asubuhi, eneo la Kata ya Bomambuzi Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, mkoani humo. ambapo sehemu ya reli hiyo ilibaki bila usalama wowote kwa usafiri wa treni, jambo ambalo linatajwa kuhatarisha maisha na kuhujumu uchumi wa usafiri wa reli nchini.

Daniel Luhalu, ni miongoni mwa mashuhuda aliyeshuhudia vijana hao waking'oa vifungio vya reli hiyo, na kuviwewka kwenye mifuko ya sambaruzi.

Luhalu alisema "Matukio ya kuibiwa kwa vifaa vya reli yameanza kushika kazi, huku baadhi ya watu wakihusishwa na biashara haramu ya vyuma chakavu."alisema.

Akiongelea swala hilo Mwenyekiti wqa CCM Wilaya ya Moshi Mjini Faraji Swai; alisema alipata taarifa kutoka wka Diwani wa Viti Maalum halmashauri ya Manispaa ya Moshi Faidha Mohamed Hamed, kuwa kuna watu walikuwa wakiharibu miundombinu ya reli.

"Baada ya kupata taarifa hizo niliwasiliana na uongozi wa serikali ngazi zote za wilaya na Mkoa ambapo walifika eneo hili, wakiwa na viongozi wa shirika la reli", alisema Swai.

Aliongeza, "Tulipofika eneo lile tulibaini kuwa tayari walishang'oa vifungio vya mataruma ya reli 95 vinavyozuia reli isitanuke jambo ambalo linaweza kusababisha treni kuanguka na kusababisha maafa makubwa kama ingepita".

Wakizungumza Diwani wa Viti Maalumu Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Faidha Mohamed Hemed na Diwani wa Kata ya Bondeni Masiwa Amiri, walisema majira ya saa tano asubuhi ya Aprili 21, 2025 walipokea taaarifa kutoka kwa raia mwema akiwaeleza kuwepo kwa watu wanaohujumu miundombinu ya reli.

Akizungumzia athari ambazo zinaweza kutokea kutokana na hujuma hizo Mkaguzi wa reli Mrisho Mohamed alisema "Vifungio hivi vinapong'olewa vinaweza kusababisha reli kutanuka na hivyo kusababisha treni kuyumba na hatimaye kuanguka".

Kwa upande wake  Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbuyuni Kata ya Bondeni Abdalla Kideko alitoa rai kwa uongozi wa reli kushirikiana na viongozi wa maeneo yanakopita reli ili kuzuia hujuma hizo.

"Kwa mfano mimi niko eneo ambalo reli inapitia lakini sijui mafundi kutoka shirika la reli hivyo akija mhujumu akaanza kugongagonga nitamwacha tu nikijua ni mhudumu wa shirika kumbe anahujumu miundombinu ya Taifa", alisema.

Aliongeza, "Ni vyema viongozi wa TRC wakashirikiana na viongozi wa mitaa kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza miundombinu ya reli na pia kutoa taariafa wakati mafundi wa shirika watakapokuja kufanya shughuli zao".

Alisema kwa kutoa taarifa za namna hiyo kutasaidia viongozi na hata wananchi kuwahoji wale ambao watakutwa wakigusa miundombinu za reli bila idhini ya shirika.

Akizungumza kwa njia ya simu Msimamizi wa miundombinu ya reli Kanda ya Kaskazini Mhandisi Mahadhi Chapanga, alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za hujuma zinazofanywa na watu wasio na nia njema na huduma zinazotolewa  na shirika hilo ili kukoa maisha ya wasafiri.

Mhandisi Chapanga, alisema uharibifu wa miundombinu hiyo mbali na kuathiri utendaji wa shirika pia unahataraisha maisha ya watu ambao hutumia usafiri wa reli kutokana na ukweli ikiharibiwa ni lazima ajali zitokee.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.