KIBO SPORTS CLUB, MONGOLA ENVIRONMENT CONSERVATION GROUP, WAPANDA MITI YA MATUNDA KUMUENZI PAPA FRANCISCO

MOSHI.

Wakati Dunia ikiombeleza kifo cha Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francisco, Wadau wa mazingira mkoani Kilimanjaro wameamua kumuenzi kiongozi huyo kwa kupanda miti kwenye uwanja wa Uhuru Park ulioko Manispaa ya Moshi, mkoani humo kama ishara ya kumuenzi kwa kazi kubwa aliyoifanya ya utunzaji wa mazingira.

Mraribu wa zoezi hilo Daniel Mvungi; alisema wameamua kupanda miti aina mbalimbali ya matunda ili kuenzi kazi nzuri aliyoifanya Papa Francisco ya kutunza mazingira wakati wa uhai wake.

"Pamoja na kazi nyingi alizokuwa akifanya ikiwemo ya kuliongoza Kanisa; Papa pia alijitoa kwa hali na mali katika kuhamasisha uboreshaji na utunzaji wa mazingira duniani kote, hivyo na sisi tumepanda miti aina mbalimbali ili kuenzi kazi alizokuwa akifanya Papa",


Mvungi ambeye ni Mwenyekiti wa taasisi isiyo ya kiserikali ya (Kibo Sports Club), inayojishughulisha na michezo na mazingira alisema, waliendesha zoezi hilo la upandaji wa miti kwa ushirikiano wa karibu na taasisi ya mazingira ya Mongola Environment Conservation Group.

Aliongeza, "Zoezi hili ni sehemu ya kazi ya kupanda miti kwa lengo la kurudishia uoto wa asili na kuboresha mazingira ambapo tangu tuanze shughuli hizi mwaka 2012 tumeshapanda zaidi ya miti 6,000 katika maeneo mbalimbali mkoani hapa".

Kwa upande wake, Mjumbe wa taasisi hiyo Hamis Mapai, alisema zoezi hilo ni kumbukumbu nzuri ya kuenzi kazi nzuri ya utunzaji wa mazingira aliyokuwa akiifanya Papa Francisco.

"Nitoe rai kwa watu wote duniani wenye kujali mazingira kumuenzi Papa Francisco kwa kuboresha mazingira maeneo wanayoishi", alisema na kuongeza, utunzaji wa mazingira ni moja ya urithi ambao Papa Francisco alituachia.


Kwa upande Mkufunzi wa masuala ya Utamaduni  ambaye pia ni Mjumbe wa taasisi ya Mongola Environment Conservation Group     Gasper Shirima Gorila, kwa jina maarufu kama Mtikisa Misitu, alitoa rai kwa wananchi kutumia mvua zinazoneysha kila mwaka kupanda miti ili kuboresha mazingira.

"Kila mwaka tunajaliwa kupata mvua za masika na za vuli lakini maji ya mvua huishia chini tu; ni vyema sasa kuanzia sasa tukajenga utamaduni wa kutumia mvua hizi kupanda miti kila mwaka", alisema, na kuongeza, hii pia itakuwa ni njia nzuri ya kumuenzi Papa Francisco ambaye wakati wa uhai wake alijikita katika kuboresha mazingira.


Baadhi ya washiriki wa zoezi hilo John Mushi, Amina Rashid na Assenga, walieleza kufurahishwa kwao na hatua ya Kibo Sports Club na Mongola Environment Conservation Group, wakisema imewapa motisha ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi wa mazingira.

Aidha waliahidi kuendelea kutunza miti hiyo na kuhamasisha wengine kuiga mfano huo mzuri, kupitia tukio hilo, ambapo mchango wa Papa Francisco katika kulinda mazingira utaendelea kukumbukwa na kuenziwa kwa vitendo vinavyoleta mabadiliko chanya katika jamii.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.