RAIA WA KIGENI 7,069 WAKAMATWA KWA UKIUKWAJI WA SHERIA ZA UHAMIAJI


DODOMA.

Idara ya Uhamiaji nchini imefanikiwa kuwakamata jumla ya raia wa kigeni 7,069 waliobainika kuishi au kufanya kazi kinyume cha sheria katika kipindi cha miezi minne ya ukaguzi maalum uliofanyika kote nchini kuanzia Januari hadi Aprili, 2025.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mrakibu Mwandamizi wa Idara ya Uhamiaji (SSI), Paul Mselle, alisema hatua mbalimbali za kisheria zimechukuliwa dhidi ya wahusika hao.

Alisema kati ya waliokamatwa, raia wa kigeni 1,008 wamefikishwa mahakamani ambapo 703 wamehukumiwa kifungo gerezani, 257 wamehalalisha ukaazi wao kwa kufuata taratibu, huku wengine 4,796 wakiondoshwa nchini. 

"Idara ya Uhamiaji inapenda kuutarifu Umma kuwa imefanya ukaguzi maalum nchi nzima kwa kipindi cha miezi minne kuanzia Januari hadi Aprili, 2025 kwa lengo la kuwachukulia hatua za kisheria raia wa kigeni ambao wanaishi, kufanya kazi nchini au biashara kinyume cha masharti ya vibali vyao,"alisema SSI Mselle.

Aliongeza kuwa "Kupitia zoezi hilo, Idara tulifanikiwa kuwakamata raia wa kigeni 7,069 kutoka katika mataifa tofauti na hatua mbalimbali zimechukuliwa dhidi yao ikiwemo watu 1,008 walifikishwa mahakamani na kati yao watu 703 walihukumiwa kifungo gerezani, 257 wamehalalisha ukaazi wao na watuhumiwa 4,796 wameondoshwa nchini, huku watuhumiwa wengine 305 uchunguzi bado unaendelea". 

Alisema Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama iliendesha operesheni maalum katika eneo la Kariakoo, Jijini Dar es Salaam, ambapo raia wa kigeni 62 kutoka mataifa mbalimbali walikamatwa na kuondolewa nchini kwa kosa la kuishi na kufanya biashara bila vibali halali ikiwemo kukiuka masharti ya vibali vyao.

Alisema kuwa hatua hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha usalama wa nchi na udhibiti wa uingiaji holela wa wageni wasiokuwa na vibali halali.

Aidha alisema kuwa Idara ya Uhamiaji inatoa rai kwa wageni wote wanaoishi au kufanya shughuli nchini kuzingatia masharti ya vibali vyao ili kuepuka mkono wa sheria katika kipindi hiki ambacho ukaguzi wa raia wa kigeni unaendelea nchini kote.

Itakumbukwa kuwa baadhi ya wafanyabiashara wa soko la Kariakoo walipaza sauti zao kwa serikali za kuwepo kwa raia wa kigeni ambao wanafanyabiashara ndogo ndogo katika maeneo hayo, biashara ambazo zilipaswa kufanywa na wazawa.

Baada ya kilio hicho kusikika serikali iliunda Kamati ya ufuatiliaji na kuhakikisha raia wa kigeni hawajihusishi na biashara zinazopaswa kufanywa na wazawa,  kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Profesa Edda Lwoga, aliyeongoza kamati hiyo  ilibaini  eneo la Kariakoo pekee kuwepo kwa maduka 75 ambayo yalikutwa na raia wa kigeni , 152 wakiwa wameajiriwa huku asilimia 97 wakijihusisha na biashara za reja reja.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.