MOSHI.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro limeadhimisha miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii katika Kituo cha Afya Majengo, kilichopo halmashauri ya Manispaa ya Moshi mkoani humo.
Shughuli hizo zimehusisha usafi wa mazingira kuzunguka kituo hicho, kugawa zawadi kwa wagonjwa waliolazwa katika wodi ya akina mama na watoto, utoaji wa vifaa vya usafi pamoja na kugawa miche ya miti kama mchango wa kulinda mazingira.
Akizungumza Aprili 26,2025, wakati wa tukio la kukabidhi vifaa hivyo, Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi, alisema katika kuadhimisha miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, wameamua kufanya shughuli mbalimbali za kijamii kituoni hapo.
Aidha alisema katika kuhamasisha utunzaji wa mazingira , Jeshi hilo pia limegawa miche ya miti kwa ajili ya kupandwa katika eneo la kituo hicho pamoja na maeneo jirani, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Majengo, Dkt. Godfrey Mariki, aliipongeza juhudi za jeshi hilo kwa moyo wa kujitolea na kushiriki katika kuboresha huduma za afya.
“Nitoe shukrani zangu za dhati kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro kwa kuona umuhimu wa kuienzi siku ya Muungano kwa kutoa zawadi mbalimbali ikiwemo vifaa vya usafi katika kituo chetu hiki,"alisema Dkt. Mariki.
Aidha alilipongeza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa huo, licha ya kufanya tu usafi lakini pia walikwenda kwenye wodi ya mama na mtoto na kuwakabidhi vifaa vya usafi kama sabuni ikiwa ni sehemu ya kuwashika mkono, sambamba na kutoa miche ya miti ambayo tutaipanda kama ishara ya Muungano huu muhimu,” alisema Dkt. Mariki.
Wakizungumza baadhi ya akina mama walijifungua katika wodi hiyo Esther Samwel na Godliver Njau, wamelishukuru Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani humo kwa kuweza kutenga muda wao na kuja kuwatembelea huku wakiziomba na taasisi zingine ziige mfano huo wa Jeshi la Zimamoto.”
Tukio hilo linatajwa kuacha alama ya mshikamano, uzalendo na huruma kwa jamii, na kuonesha namna ambavyo taasisi za serikali zinaweza kushiriki katika maendeleo ya kijamii kwa vitendo.