MOSHI.
Katika kuadhimisha miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro limewapatia elimu ya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto watumishi wa Kituo cha Afya Majengo , ikiwa ni sehemu ya jitihada za kulinda maisha na mali ya wananchi.
Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo watumishi hao kukabiliana na majanga ya moto kazini na majumbani, sambamba na kuwafundisha namna sahihi ya kutumia vifaa vya kuzimia moto.
Akizungumza katika tukio hilo, Kamanda wa Jeshi hilo, Mrakibu Msaidizi Jeremiah Mkomagi Kamim alisema, waliamua kutoa elimu hiyo kwa watumishi hao namna ya kutumia vifaa vya kuzimia moto, hatua za kuchukua wakati wa dharura, na mbinu za kujiokoa pindi ajali ya moto inapotokea.
“Jeshi limeweza kutoa elimu ya zimamoto kwa wenzetu wa hospitali, ambayo itawasaidia katika udhibiti wa majanga pindi yanapotokea, tunafahamu wafanyakazi hawa wana makazi yao na hutumia majiko ya gesi na moto hauchagui utokee wapi, hivyo kwa elimu hii itawawezesha kuwafundisha na wengine kwenye maeneo yao ya kazi na makazi yao pia.”
Mbali na elimu hiyo, Jeshi hilo lilifanya usafi katika mazingira ya kituo, kutoa zawadi kwa wagonjwa waliolazwa, hususan katika wodi ya akina mama na watoto, sambamba na kugawa vifaa vya usafi na miche ya miti kwa ajili ya kulinda mazingira.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Majengo, Dkt. Godfrey Mariki, aliunga mkono hatua hiyo na kueleza umuhimu wake.
"Eneo tunalofanyia kazi linagusana na majanga tofauti, tunayo miundombinu ya umeme, tuna gesi, na hata majumbani tunakokaa, kwa elimu hii tuliyopewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, itatusaidia sana kuweza kudhibiti majanga ya moto kwenye maeneo tunayofanyia kazi pamoja na makazi yetu.”
Aidha, Dkt. Mariki aliishukuru Zimamoto kwa msaada wa zawadi kwa wagonjwa na vifaa vya usafi, akisema kuwa juhudi hizo zimeonesha namna taasisi za serikali zinavyoweza kushiriki moja kwa moja katika kuboresha huduma za kijamii.