BUNGENI-DODOMA.
Serikali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI, imeagiza Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, kuhakikisha anapeleka vifaa tiba katika Kituo cha Afya Umbwe, kilichopo katika Jimbo la Moshi Vijijini, kwa kutumia fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya huduma za afya.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Zainab Katimba (Mb), wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi, katika kikao cha Bunge kilichofanyika Aprili 25 mwaka huu, Jijini Dodoma.
Katika swali lake, Prof. Ndakidemi alihoji mpango wa serikali katika kuhakikisha Kituo cha Afya Umbwe, ambacho ni kituo pekee cha afya katika Tarafa ya Kibosho yenye kata sita, kinapatiwa vifaa tiba kutokana na upungufu mkubwa uliopo.
“Kituo cha afya Umbwe kina upungufu mkubwa sana wa vifaa tiba. Je, Serikali ina mkakati gani wa kusaidia kituo hiki ili wananchi waweze kupata huduma bora za afya?” alihoji Mbunge huyo.
Akijibu, Mhe. Katimba alisema kuwa serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya afya, ambapo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Awamu ya Sita, jumla ya shilingi trilioni 1.29 zimetolewa kwa ajili ya kuboresha huduma za afya ya msingi kote nchini.
Naomba nimhakikishie Mbunge Profesa Ndakidemi kuwa serikali imeshatuma fedha nyingi katika kila halmashauri kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba.
"Nitumie fursa hii kwa niaba ya Waziri Ofisi ya Rais (TAMISEMI), kumwagiza Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO) kutumia fedha alizopokea katika mwaka wa fedha 2024/2025 kuhakikisha ananunua vifaa tiba kwa ajili ya kupeleka katika Kituo cha Afya Umbwe,” alisema Naibu Waziri Katimba.