NJORO-MOSHI.
Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Priscus Tarimo, amewakaribisha makada wa chama hicho, wanaotamani kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao, huku akisisitiza kuwa yupo tayari kwa ajili ya kupimana ubavu kisiasa kwa misingi ya kazi na sio maneno.Kwa sasa kampeni za chini chini zimeanza kushika kasi katika jimbo hilo, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, huku baadhi ya majina mapya yakitajwa kutaka kuwania nafasi ya ubunge kupitia chama hicho.
Tarimo aliyasema hayo jana wakati akizungumza kwenye mkutano wa viongozi wa wa CCM ngazi ya matawi, kata na wilaya ulioitishwa na sekretarieti ya CCM mkoa wa Kilimanjaro, kwa lengo la kutoa mafunzo kwa wajumbe wa mkutano mkuu maalum walioongezwa ngazi ya wilaya na kata.
Alisema katika ahadi 10 alizoziahidi wakati wa kampeni za kuwaomba ridhaa wananchi kuwa mwakilishi wao mwaka 2020, ahadi 9 zimetekelezwa huku akibakiwa na ahadi moja ya mji wa Moshi kuwa Jiji.
Alisema miongoni mwa ahadi alizoziahidi ni pamoja na ujenzi wa uwanja wa mpira, ujenzi wa shule mpya za sekondari, ujenzi wa hospitali ya Wilaya, ukarabati wa uwanja wa ndege Moshi, uboreshaji wa barabara za lami na maendeleo mengine ya kijamii na kiuchumi.
"Nafahamu wako watu wameanza kujipitishapisha kutaka kugombea ubunge katika Jimbo hili, ninawakaribisha sana wote mje tupimane ubavu, nilitumwa kazi ya kuwaletea maendeleo Moshi mjini na baadhi ya ahadi zangu zimetekelezwa kikamilifu, na haya ni matokeo ya kodi zenu na si fedha za mtu binafsi," alisema Tarimo.
Aidha mbunge huyo aliwataka wananchi na makada wa chama hicho, wakati utakapofika kumpima kwa kazi alizozifanya badala ya kushawishika na watu wanaozunguka kwa madai ya ‘kutumwa na viongozi kutoka juu’.
"Wako wanaozunguka wakiwa na fedha, lakini mwisho wa siku kazi ya mbunge sio kugawa hela, bali kuhakikisha kodi zenu zinatumika vizuri, Bunge likivunjwa, narudi tupimane ubavu," alisema.
Aliongeza kuwa "Mimi mtanituma nyie, sio mtu mwingine, maendeleo ya nchi tangu uhuru yanaletwa kwa fedha za wananchi kupitia kodi, si fedha kutoka mfukoni kwa mtu, hata aje nani, mwisho wa siku kazi yake ni kupambana Bungeni ili fedha hizo ziletwe.....Si kila mtu ana uwezo wa kuongoza,"alisema Tarimo.
Alisema "Kila mtu Mungu amempa karama yake, kuna anayejua riadha, mwingine mpira wa miguu; kuna mtaalamu wa udaktari, mwingine biashara; hivyo kila mmoja atatambua mafanikio kulingana na tunu aliyopewa."
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, akizungumza kwenye mkutano wa Viongozi wa CCM ngazi ya Matawi, Kata na Wilaya ulioitishwa na sekretarieti ya CCM mkoa wa Kilimanjaro, uliofanyika Kata ya Njoro kwa lengo la kutoa mafunzo kwa wajumbe wa mkutano mkuu maalum walioongezwa ngazi ya wilaya na Kata.
Diwani wa Kata ya Miembeni Manispaa ya Moshi, Mohamed Mushi, akimtunza Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Priscus Tarimo, wakati wa mkutano wa Viongozi wa CCM ngazi ya Matawi, Kata na Wilaya ulioitishwa na sekretarieti ya CCM mkoa wa Kilimanjaro, uliofanyika Kata ya Njoro kwa lengo la kutoa mafunzo kwa wajumbe wa mkutano mkuu maalum walioongezwa ngazi ya wilaya na Kata.
Apaikunda Naburi Diwani wa Kata ya Mawenzi, akizungumza kwenye mkutano wa Viongozi wa CCM ngazi ya Matawi, Kata na Wilaya ulioitishwa na sekretarieti ya CCM mkoa wa Kilimanjaro, uliofanyika Kata ya Njoro kwa lengo la kutoa mafunzo kwa wajumbe wa mkutano mkuu maalum walioongezwa ngazi ya wilaya na Kata.
Diwani wa Kata ya Kaloleni Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Nasib Mariki, akizungumza kwenye mkutano wa Viongozi wa CCM ngazi ya Matawi, Kata na Wilaya ulioitishwa na sekretarieti ya CCM mkoa wa Kilimanjaro, uliofanyika Kata ya Njoro kwa lengo la kutoa mafunzo kwa wajumbe wa mkutano mkuu maalum walioongezwa ngazi ya wilaya na Kata.