ELIMU, AFYA NA UWEZESHAJI: MATUNDA YA BILIONI 32.8 KUTOKA KWA RAIS SAMIA

NJORO-MOSHI.

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, amesema kuwa ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Manispaa ya Moshi imenufaika kwa kiasi kikubwa kwa kupokea Shilingi bilioni 32.8 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.


Akizungumza jana kwenye mkutano wa viongozi wa CCM ngazi ya matawi, kata na wilaya ulioitishwa na sekretarieti ya CCM mkoa wa Kilimanjaro uliofanyika Kata ya Njoro, Mnzava alisema fedha hizo ni kutoka Serikali Kuu pamoja na mapato ya ndani ya halmashauri, na zimetumika kutekeleza miradi ya elimu, afya, na uwezeshaji wananchi kiuchumi.


“Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 22 zimetolewa na Serikali Kuu, na Sh bilioni 10 ni kutoka mapato ya ndani ya Manispaa, tumefanikisha ujenzi wa shule mpya nne za sekondari, tumekarabati madarasa 71, na tumejenga na kukarabati matundu ya vyoo 280,” alisema Mnzava.

Aidha, alibainisha kuwa halmashauri kupitia mapato yake ya ndani imetoa mikopo ya zaidi ya Sh milioni 576 kwa wananchi ili kuwawezesha kiuchumi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupambana na umasikini.

Katika hotuba yake, Mnzava aliwahimiza wananchi kuendelea kudumisha amani, upendo na utulivu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais.

Akizungumzia uchaguzi unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, alisema kuna baadhi ya watu wanataka kuwanyima wananchi haki yao ya kuchagua na kuchaguliwa, ambayo ni haki ya kikatiba, lakini akaonya kuwa watu hao hawapaswi kupewa nafasi.


“Katiba yetu inaeleza wazi kuwa kila baada ya miaka mitano tunapaswa kurudi kwa wananchi ili wachague viongozi wanaowataka, , hakuna mamlaka yoyote inayoweza kuzuia uchaguzi huu usifanyika,” alisema.

Alisisitiza kuwa Wilaya ya Moshi iko tayari kwa uchaguzi wa huru na haki, na Tume Huru ya Uchaguzi imejipanga kuhakikisha mchakato huo unakwenda vizuri.


Akizungumza Mwenyakiti wa CCM Moshi mjini Faraji Swai, alisema katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, wamejipanga kikamilifu kuirejesha kata ya kiboriloni iliyoko Chadema.
 
"Iwe jua, iwe mvua CCM tutakwenda kupiga kambi kata ya kiboriloni na mimi mwenyewe binafsi nitaongoza kundi hili na hatuna utani kata ile lazima mwaka huu tuivalishe bendera ya kijani."






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.