MBUNGE NDAKIDEMI AHOJI SERIKALI KUHUSU UHABA WA VITUO VYA ZIMAMOTO MOSHI VIJIJINI

DODOMA.

Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi, ameuliza swali la nyingongeza Bungeni akitaka kufahamu mkakati wa Serikali katika kuimarisha huduma za zimamoto katika maeneo ya vijijini, hususan ngazi ya Tarafa.

Katika swali lake, Profesa Ndakidemi alisema kuwa ajali za moto zimekuwa zikitokea mara kwa mara katika Jimbo hilo na kwamba mara nyingi askari wa zimamoto hufika kwa kuchelewa kutokana na umbali mkubwa kutoka vituo vyao hadi maeneo ya matukio.

Alisema kwa muda mrefu, wakazi wa maeneo ya vijijini nchini wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma za haraka za zimamoto, jambo linalochangia kuongezeka kwa madhara ya moto katika jamii.

“Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha vituo vya zimamoto katika ngazi ya Tarafa ili wananchi waweze kupata huduma kwa wakati?” alihoji Profesa Ndakidemi.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Baran Sillo (Mb.), alisema Serikali inatambua changamoto hiyo na inaendelea na jitihada za kupanua huduma za zimamoto nchini kote kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mhe. Sillo alibainisha kuwa Serikali iko katika hatua ya kufanya tathmini ya mahitaji ya kila Tarafa ili kuandaa mpango wa kuanzisha vituo vya zimamoto vinavyokidhi mahitaji ya wakazi wa maeneo husika.

“Tunaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali Kuu na Halmashauri katika kuhakikisha huduma hizi zinawafikia wananchi kwa haraka na kwa ufanisi,” alisema Naibu Waziri.

Hatua hii inatajwa kulenga kupunguza madhara yanayosababishwa na moto katika maeneo ya vijijini na kulinda maisha pamoja na mali za wananchi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.