Walimu wampongeza Rais Samia kwa maboresho sekta ya elimu

MOSHI-MANISPAA.

Jukwaa la Waalimu Wazalendo Tanzania (JWW) Manispaa ya Moshi mkoa wa Kilimanjaro, wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujenga msingi imara wa maboresho katika  sekta ya elimu nchini.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Walimu Wazalendo Manispaa ya Moshi Mwl Rashid A. Rashidi ameyasema hayo Januari 25, 2025 wakati akizungumza kwenye Kongamano la kufungua mwaka wa masomo 204/2025, lililofanyika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro.

Amesema tangu Rais Samia alipoingia madarakani Machi 19,2021, amefanya maboresho makubwa kwenye sekta ya elimu ikiwemo yale ya kisera na kimuundo huku akiwekeza zaidi katika ujenzi wa miundombinu hatua ambayo imeleta unafuu kwa Watanzania.

“Tunampongeza na kumshukuru sana Rais Samia na kwa juhudi zake za kuboresha miundombinu ya elimu nchini ikiwemo ujenzi wa madarasa,” amesema Mw. Rashid.

Mwalimu Rashid ambaye pia ndie Afisa elimu Kata ya Bondeni Manispaa ya Moshi. Amesema kuwa pia serikali imepandisha madaraja na kulipa viwango vipya vya mishahara ambapo  huko nyuma halikufanyika.

Alisema kupitia maboresho hayo walimu wameendelea kutekeleza majukumu yao kikamilifu kwa kupandisha viwango vya ufaulu kwa shule za msingi na sekondari.

Naye Mwl. Doroth Mmbaga kutoka shule ya Awali na Msingi Shaurimoyo, amesema  kuboreshwa kwa miundombinu ya elimu kwa kujenga na kukarabati madarasa, imefanikisha Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kuendelea kushika namba moja katika ufaulishaji wa wanafunzi.

“Ndani ya miaka mitatu Rais Samia amefanya mengi tunayojivunia na yamekuwa msingi katika kuboresha sekta yetu ya aelimu,”alisema.

Aidha alisema jambo jingine wanalojivunia kama walimu ni kufuta ada  kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita ili kumpunguzia mzigo wa gharama wazazi na walezi wa wanafunzi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mwl. Mwajuma Nasombe, Amesema ndani ya miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais Samia Manispaa ya Moshi imepokea fedha za miradi ya maendeleo Sh bilioni 32.

Mwl. Nasombe alisema kwenye sekya ya elimu Manispaa hiyo ilipokea Sh bilioni 14.3, ambapo idara ya elimu sekondari  walipokea Sh bilioni 10.8  huku sekta ya elimu Msingi wakipokea Sh bilioni 3.5.

Aidha amesema kwa kipindi hicho pia walifanikiwa kujenga shule mpya nne, shule tatu zikiwa za sekondari na moja elimu msingi.

“Tumetumia Sh bilioni 2.07 kujenja shule mpya za kisasa,lakini pia tumefanikiwa kujenga madarasa 112  yenye thamani ya Sh bilioni 2.47, matundu ya vyoo 305 yenye thamani y ash milioni 532. Mabweni 6 yenye thamani ya Sh milioni 870.

Vilevile alisema kati ya fedha hizo wamejenga mabweni sita, mabweni manne yamejengwa na fedha za Serikali Kuu huku mabweni mawili kwa yakijengwa kwa kutumia fedha za mapato ya ndani.

Aidha amesema wamefanya ukarabati wa shule kongwa kwa Sh milioni 500 na kati ya fedha hizo zipo ambazo zimetoka Serikali kuu na zingine zinatokana na mapato ya ndani.

“Pia tumejenga nyumba tatu za walimu zenye thamani ya Sh milioni 231, hivyo tunamshukuru na kumpongeza sana Rais Samia  kwa kuishika mkono sekta hii.”alisema Mwl. Nasombe.

Akifungua kongamano hilo Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, amempongeza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Mwl. Mwajuma Nasombe kwa kuja na wazo la kujenga bweni la watoto wa kiume ili kukabiliana na ukatili wanaofanyiwa kwenye jamii, ikiwemo vitendo vya ulawiti.

“kwa sasa ukiangalia matukio mengi ya ulawiti yanayotokea hivi sasa dhidi ya watoto wa kiume ni makubwa sana, kujenga kwa bweni hili itakuwa ni usalama mkubwa kwa watoto wetu wa kiume."alisema RC Babu.

Katika Kongamano hilo Walimu hao pia walifundishwa kuhusiana na Masuala ya Ulinzi na Usalama wa mtoto kutoka Jeshi la Polisi, Utumiaji Nishati Safi ya kupikia, Nidhamu, Maadili sambamba na Masuala ya Maslahi ya Walimu semina iliyotolewa na Katibu wa TSC Manispaa ya Moshi.






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.