MAKUYUNI WILDLIFE PARK IMEANDAA SAFARI MAALUM KWA WASHIRIKI WA TAMASHA LA MAGARI YA ZAMANI MOSHI-KILIMANJARO.

HIFADHI ya Makuyuni Wildlife Park imetangaza kuandaa safari maalum ya utalii wa ndani kwa washiriki wa Tamasha la Magari ya Zamani litakalofanyika Desemba 28, mwaka huu, ikiwa ni hatua ya kuhamasisha na kukuza utalii wa ndani.

Afisa Utalii wa Makuyuni Wildlife Park, Mustafa Buyogera, ameyasema hayo Novemba 28, 2025 mjini Moshi wakati wa mahojiano na waandishi wa habari mara baada ya uzinduzi wa tamasha hilo uliofanyika katika Viwanja vya Posta.

Buyogera alisema hifadhi hiyo inayosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeamua kushiriki katika tamasha hilo kutokana na kuona fursa kubwa ya kuwafikia Watanzania na kuwahamasisha kutembelea vivutio vya ndani.

Alisema safari hiyo maalum itakayofanyika Desemba 30 imeandaliwa mahsusi kwa washiriki wote wa tamasha hilo ili kuwapa nafasi ya kutembelea Hifadhi ya Miakuyuni na kujionea vivutio vya asili vya nchini.

“Kwetu sisi kama TAWA, kushiriki uzinduzi wa Tamasha la Magari ya Zamani ni fursa kubwa. Tumeamua kuandaa safari ya washiriki ili kuongeza hamasa ya utalii wa ndani,” alisema Buyogera.

Alifafanua kuwa tamasha hilo limevutia watu wengi waliokuja kuona magari ya zamani ya kuanzia miaka ya 1950, 1960 na 1970, ambayo yamekuwa kivutio kipya kwa wakazi wa Kanda ya Kaskazini na kuongeza aina mpya ya utalii nchini.

“Ni aina mpya ya utalii, watu wanapata historia ya magari, uimara wake na jinsi yalivyotumiwa, hii itasaidia kuongeza mwamko wa utalii wa ndani,” aliongeza.

Kwa upande wake, Afisa Utalii Kitengo cha Picha katika Eneo la Ziwa Natron, Rosmina Mshana, aliwataka Watanzania kuondoa dhana ya kuwa utalii ni kwa wageni pekee na kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya ndani.

Alisema gharama za kutembelea vivutio hivyo ni nafuu, akieleza kuwa kiingilio cha kutembelea Ziwa Natron kwa Mtanzania ni Sh 8,260, hivyo wananchi wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo.

“Gharama zetu ni nafuu, tunawakaribisha Watanzania kutembelea mbuga zetu na kujionea vivutio vya pekee, ikiwemo utalii wa picha unaovutia wageni wengi kutoka duniani,” alisema Mshana.

Alisisitiza kuwa vivutio vya Ziwa Natron na Hifadhi ya Makuyuni vinaendelea kupokea wageni kutoka mataifa mbalimbali, hivyo ni muhimu Watanzania pia wakajitokeza kuvitembelea.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.