MOSHI-KILIMANJARO
NCHI tano za Kenya, Botswana, Uganda, Afrika Kusini na Rwanda zimeonyesha nia ya kushiriki katika tamasha kubwa la maonesho ya magari ya zamani lijulikanalo kama Kilimanjaro Classic Car Show and Adventurer Trip, linalotarajiwa kufanyika Desemba 28 mwaka huu.
Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa tamasha hilo uliofanyika katika viwanja vya Posta mjini Moshi, Mkurugenzi wa African Sports Agency Company Ltd, Joseph Mselle, alisema lengo la tamasha hilo ni kuanzisha na kukuza utalii wa maonesho ya magari ya zamani katika mkoa wa Kilimanjaro.
“Tuko hapa kwa ajili ya uzinduzi wa tamasha la maonesho ya magari ya zamani katika mkoa wetu wa Kilimanjaro kwa msimu wa kwanza,” alisema Mselle.
Mselle alifafanua kuwa mkoa wa Kilimanjaro ni miongoni mwa maeneo nchini yenye idadi kubwa ya magari ya zamani, na hadi sasa magari 13 ya aina mbalimbali yakiwemo Land Rover, Datsun, Peugeot na Suzuki yamejisajili kushiriki.
Aliongeza kuwa wanatarajia zaidi ya magari 300 kushiriki katika maonesho hayo, ambayo pia yatatoa fursa mbalimbali za kibiashara katika viwanja vya Mashujaa, vitakavyotumika kwa mashindano.
Akizindua rasmi tamasha hilo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa, aliwapongeza waandaaji kwa hatua ambayo alieleza kuwa itachochea maendeleo ya kiuchumi kupitia utalii.
“Kuwepo kwa tamasha hili kunautangaza mkoa wetu wa Kilimanjaro ndani na nje ya nchi. Wageni kutoka mataifa mbalimbali watakuja kushuhudia magari yaliyotengenezwa miaka mingi iliyopita lakini bado yapo katika hali nzuri na yanafanya kazi,” alisema Nzowa.
Aliongeza kuwa tamasha hilo litakuwa kivutio kikubwa cha utalii wa ndani, kwani wageni watakaohudhuria watatumia huduma za usafiri, malazi na chakula, hivyo kuongeza pato la mkoa na la wananchi kwa ujumla.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, alisema kufanyika kwa tamasha hilo ndani ya wilaya kutawapa fursa wajasiriamali kufanya biashara zao.
Alisema pia washiriki watapata fursa ya kujifunza kuhusu utunzaji wa magari ya zamani, elimu ya usalama barabarani, pamoja na kushuhudia wataalamu kutoka Chuo cha VETA wakionyesha stadi mbalimbali.













