MOSHI-KILIMANJARO.
TAKRIBANI magari 300 ya zamani yanatarajiwa kuonyesha mvuto wao katika Tamasha la Kilimanjaro Classic Car Show and Adventurer Trip linalotarajiwa kufanyika Desemba 28 mjini Moshi, mkoa wa Kilimanjaro.
Tamasha hilo limevutia washiriki kutoka nchi tano za Afrika, zikiwemo Kenya, Uganda, Botswana, Afrika Kusini na Rwanda.
Mkurugenzi wa African Sports Agency Company Ltd, Joseph Mselle, ameyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa tamasha hilo katika viwanja vya Posta,
Alisema lengo ni kukuza utalii wa maonesho ya magari ya zamani na kuutangaza zaidi mkoa wa Kilimanjaro.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa, aliwapongeza waandaaji kwa hatua ya kuleta tukio kubwa la kimataifa katika mkoa huo.
Alisema tamasha hilo litachangia kwa kiasi kikubwa kutangaza mkoa ndani na nje ya nchi kupitia wageni watakaofika kushuhudia magari hayo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, alisema tamasha hilo litawapa wajasiriamali wa eneo hilo nafasi ya kipekee ya kufanya biashara.








