CCM KILIMANJARO YAMPONGEZA RAIS SAMIA KWA HOTUBA YENYE KUIMARISHA AMANI, MSHIKAMANO

MOSHI-KILIMANJARO.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro kimempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa hotuba aliyotoa Desemba 2, 2025 alipokutana na wazee wa Jiji la Dar es Salaam, wakisema imeleta mwanga na dira mpya katika kipindi ambacho taifa linahitaji umoja na utulivu.

Akizungumza kupitia taarifa yake kwa waandishi wa habari, Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Abraham Urio, alisema hotuba hiyo imejaa hekima na kuonyesha kuwa Tanzania inaendelea kuongozwa na falsafa ya “Umoja ni Nguvu, Utengano ni Udhaifu.”

“Hotuba ile imesimama kama taa ya mwanga katika kipindi hiki ambacho taifa letu linahitaji amani, mshikamano na mwelekeo mmoja kitaifa,” alisema Urio.

Alibainisha kuwa hotuba ya Rais Samia imesisitiza ukweli ulio wazi kwa Watanzania wengi kwamba hakuna maendeleo bila amani. “Amani inatoa fursa ya watu kufanya kazi na familia kuishi kwa utulivu; hii ndiyo Tanzania tunayoitaka,” aliongeza.

Urio alisema uongozi wa CCM mkoani humo unaunga mkono wito wa Rais Samia kwa viongozi wa dini kuendelea kuhimiza umoja miongoni mwa Watanzania, akieleza kuwa viongozi hao wana nafasi muhimu kutokana na ukaribu wao na waumini.

Aidha, aligusia umuhimu wa wazee kukaa na vijana ili kuwaelimisha thamani ya amani waliyoikuta na wanayotakiwa kuilinda.

“Tamko hili ni la hekima, hasa ikizingatiwa nafasi ya wazee katika kuhubiri umoja, upendo na maadili mema, na kuwajenga vijana ambao mustakabali wao unategemea amani na utulivu wa nchi,” alisema.

Akitaja moja ya hoja zingine za hotuba hiyo, Urio alisema imehimiza umuhimu wa Watanzania kujenga tabia ya kusikilizana na kushauriana badala ya kushindana.

“Hili ni muhimu kwani kusikilizana kunatupa fursa ya kujenga msingi wa taifa linalojadiliana kwa hekima kwa ajili ya maendeleo yake,” alisema.

Aliongeza kuwa hotuba ya Rais Samia imefundisha kuwa uvumilivu na upendo ndiyo msingi wa mabadiliko ya kweli na ni silaha muhimu katika kulinda taifa wakati wa changamoto.

Urio alitoa wito kwa Watanzania kuendeleza elimu ya thamani ya amani na kuepuka lugha za chuki, hususan zile zinazoenea kupitia mitandao ya kijamii.

“Tuijenge Tanzania yenye upendo, heshima na Utu,” alisema.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.