SIHA-KILIMANJARO.
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Siha limewataka viongozi na watumishi wa umma kuacha kutumia madaraka yao kuwaumiza wananchi, likisisitiza kuwa vitendo vya uonevu na matumizi mabaya ya madaraka havitavumiliwa.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Duncan Urassa, wakati wa kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani baada ya kuapishwa rasmi kuanza kazi. Alisema katika kipindi kilichopita kumekuwepo na malalamiko ya wananchi na watumishi kuonewa kutokana na matumizi mabaya ya madaraka.
“Watu wasitumie nafasi zao za kimamlaka kuwaumiza wengine, kama nitaendelea kuwepo hapa halmashauri, sitaki kusikia mtu ameumizwa,” alisema Urassa.
Aliongeza kuwa maamuzi yote yaliyopitishwa na Baraza la Madiwani lililopita lakini hayajatekelezwa hadi sasa, hususan yanayohusu haki za watumishi walioonewa, yatafanyiwa kazi, na hatua zitachukuliwa dhidi ya watumishi watakaobainika kukaidi maamuzi ya baraza.
Urassa alisema kabla ya baraza lililopita kuvunjwa, kulitolewa maagizo mbalimbali ambayo hayakutekelezwa hali, iliyosababisha baadhi ya watumishi kudaiwa kuiba fedha za halmashauri bila ushahidi na kuadhibiwa kinyume cha haki.
Alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maagizo hayo katika kikao kijacho cha baraza kitakachofanyika Desemba 18 mwaka huu, akisisitiza kuwa mtumishi yeyote aliyeonewa anatakiwa kurejeshwa kazini na kutendewa haki.
“Sisi kama baraza tulidanganywa na kumwadhibu mtumishi, halafu aliyekuwa akitupa taarifa hizo akaondoka na kutuachia mzigo. Hili haliwezi kukubalika hata mbele ya Mwenyezi Mungu,” alisema.
Aidha, Mwenyekiti huyo aliwataka madiwani kuwajibika kikamilifu katika kata zao, wakuu wa idara za elimu msingi na sekondari pamoja na afya, akisema uwajibikaji huo utaongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.
Pia alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa uwazi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hususan katika maeneo ya vijijini, huku akipongeza hatua ya Mkurugenzi Mtendaji kuwasilisha taarifa ya madeni ya halmashauri kwa uwazi, jambo ambalo halikuwahi kufanyika katika baraza lililopita.
Hata hivyo, alibainisha kuwepo kwa changamoto katika baadhi ya miradi inayosimamiwa na halmashauri, akitolea mfano mradi wa utengenezaji wa tofali, akimtaka mkurugenzi kukaa na wataalamu wake wakiwemo mwanasheria, afisa manunuzi na mhandisi ili kuboresha usimamizi wa mradi huo.
Urassa alionya dhidi ya ubadhirifu wa fedha za umma akisema baraza halitaruhusu tena fedha za halmashauri kuishia mifukoni mwa watu wachache, na yeyote atakayebainika kuhujumu fedha za umma atachukuliwa hatua za kisheria.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo, ali.pongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Siha kwa kazi nzuri aliyofanya katika kipindi kifupi ambacho amekuwepo katika halmashauri hiyo kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo, hususan katika sekta ya elimu msingi na sekondari.









