SIHA-KILIMANJARO.
HOSPITALI Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto, imeanzisha mradi wa bustani ya mbogamboga na miti ya matunda kwa lengo la kuwawezesha wagonjwa wa Kifua Kikuu Sugu (TB Sugu) kujipatia kipato, kuimarisha afya ya akili na kusaidia matibabu yao wanapokuwa hospitalini kwa muda mrefu.
Afisa Ustawi wa Jamii wa hospitali hiyo, Wazoel Yohana Mshana, aliyasema hayo jana, wakati akiutambulisha mradi huo kwa waandishi wa habari.
Alisema mradi huo umeanzishwa ili kuwasaidia wagonjwa kuwa na utulivu wa afya ya akili, jambo ambalo ni muhimu sana katika matibabu ya Kifua Kikuu.
Mshana alisema matibabu ya Kifua Kikuu Sugu yanahitaji ustahimilivu mkubwa wa akili, hasa kutokana na ratiba ndefu na nzito ya matumizi ya dawa, ambapo wagonjwa wasipokuwa na utulivu wa akili huwa vigumu kufuata ratiba sahihi ya matibabu.
“Tumeamua kuanzisha mradi wa bustani ya mbogamboga na miti ya matunda ili wagonjwa waweze kufanya shughuli za uzalishaji, kupata mazoezi ya viungo na kuwa na utulivu wa akili, ambao ni sehemu muhimu ya matibabu yao,” alisema Mshana.
Aliongeza kuwa mradi huo umewezeshwa kwa ufadhili kutoka kwa wadau wa Maendeleo wa LH-International kutoka nchini Norway, ambao wametoa fedha za kuanzisha bustani hiyo.
"Kupitia mradi huu, wagonjwa wa TB Sugu waliopona hujishughulisha na kilimo kama sehemu ya mazoezi ya viungo na tiba ya kisaikolojia."alisema.
Mshana alisema tangu kuanzishwa kwa mradi huo, kumekuwa na matokeo chanya ikiwa ni pamoja na kuwajengea wagonjwa uwezo wa kujitegemea kiuchumi, huku wakipata kipato kidogo wanachokitumia kwa mahitaji binafsi na kusaidia familia zao walizoziacha nyumbani.
“Mbali na kupata kipato, wagonjwa hawa wanapata ujuzi wa kilimo cha mbogamboga na miti ya matunda, jambo litakalowasaidia hata wanaporejea katika familia na jamii zao,” alisema.
Akizungumzia mradi wa miche ya matunda Mshana alisema ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa hospitalini hapo, ambapo miti ya ndizi, maembe, parachichi na sitofeli hulimwa kwa ajili ya chakula na kipato.
Kwa upande wake, Jely Seleman Mgala, mkazi wa Mbozi mkoani Mbeya ambaye anaendelea kupata matibabu ya Kifua Kikuu katika hospitali hiyo, alisema mradi wa bustani umewasaidia sana wagonjwa tofauti na awali walipokuwa wakikaa bila kufanya shughuli za kujiongezea kipato wala mazoezi ya viungo.
“Tunaishukuru hospitali ya Kibong’oto, kwa kuanzisha mradi huu wa bustani, hapo awali tulikuwa tunakaa tu bila kufanya mazoezi, lakini sasa tunapata mazoezi, chakula na fedha kidogo kutokana na mauzo ya mbogamboga,” alisema Mgala.
Mkazi mwingine, Emanuel Paulo Mazengo kutoka Kibaigwa mkoani Dodoma, alisema mradi huo unawasaidia kupata mazoezi ya mwili, chakula bora pamoja na kipato, hali inayochangia kuimarika kwa afya zao kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto, Dk. Leonard Subi, alisema shughuli za bustani ni sehemu ya matibabu kwa wagonjwa wa TB sugu wanaoanza kupona.
Dk. Subi alisema wagonjwa hao hushiriki katika kumwagilia bustani, kupalilia na kung’oa magugu kama sehemu ya mazoezi ya kimatibabu.
“Mradi wa bustani ya mbogamboga ni sehemu ya tiba kwa wagonjwa wa TB Sugu wanaoanza kupona, unawasaidia kimwili, kiakili na kiuchumi,” alisema Dk. Subi.
Aliongeza kuwa hospitali imeanzisha mradi huo kutokana na ukweli kwamba wagonjwa wengi wa TB sugu wanatoka katika familia maskini, hivyo mradi huo unawaletea fursa ya kujipatia kipato hata wanaporejea nyumbani.
“Lengo letu ni kuona wagonjwa hawa wanakuwa na ujuzi wa kujitegemea kiuchumi hata baada ya kumaliza matibabu na kurejea kwenye familia zao,” alisema.





.jpg)


.jpg)