MWANGA MARATHON YATOA MISAADA KITUO CHA AFYA KISANGARA

Mkurugenzi wa Mwanga Marathon, Bi. Frida Mbelesero, akimkabidhi zawadi mmoja wa akina mama, aliyelazwa  Kituo cha Afya Kisangara akisubiria  muda kufika wa kujifungua.

KISANGARA-MWANGA.

Kampeni ya Mwanga Marathon & Festival imeendelea kugusa maisha ya wananchi baada ya kutoa msaada wa bidhaa mbalimbali kwa akinamama wajawazito na wale wenye watoto wachanga waliolazwa katika Kituo cha afya Kisangara, kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.

Mkurugenzi wa Mwanga Marathon, Frida Mbelesero, aliongoza tukio hilo kwa kukabidhi misaada hiyo iliowajumuisha akina mama waliopo wodini wakisubiri kujifungua, ambapo bidhaa zilizotolewa ni pamoja na taulo za kike, sabuni, mafuta ya kupaka na vifaa vingine vya msingi vinavyosaidia kujikimu hospitalini.

“Lengo letu ni kuwafariji kina mama na kuwasaidia kidogo katika kipindi hiki muhimu cha ujauzito na kujifungua, pia tunawahimiza wananchi kujali mazingira yao kwa kushiriki kwenye usafi na upandaji wa miti,” alisema Frida.

Tukio hilo liliambatana pia na shughuli za kijamii kama vile usafi wa mazingira na upandaji wa miti katika eneo la kituo hicho, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya na mazingira.

Wadau walioungana na Mwanga Marathon ni pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Wilaya ya Mwanga, waliotoa miti 200 kwa ajili ya kupandwa, KIWAMWAKU Foundation, Shirika linalopambana na mabadiliko ya tabianchi, AL BAYANU ECO Services Ltd taasisi inayojihusisha na usafi na utunzaji wa mazingira, pamoja na Chuo cha Ustawi wa Jamii Kisangara.

Akizungumza Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kisangara, Dk. Juma Kombo, aliwashukuru Mwanga Marathon kwa mchango wao muhimu kwa wagonjwa, na akaomba mashirika mengine kuiga mfano huo.

“Tumefurahi sana kutembelewa na kupata misaada hii, pia tunashukuru kwa usafi na upandaji wa miti, tunaomba wadau wengine nao wajitokeze kuunga mkono huduma za afya,” alisema Dk. Kombo.

Aidha, Dk. Kombo alitaja changamoto kubwa zinazolikabili kituo hicho kuwa ni ukosefu wa uzio unaohatarisha usalama wa vifaa na wagonjwa, uhaba wa gari la wagonjwa, hali inayochelewesha huduma kwa majeruhi na wagonjwa wa rufaa pamoja na ukosefu wa mashine ya X-ray, licha ya kituo hicho kuwa barabarani na kupokea majeruhi wengi.

“Tunaomba msaada wa gari la wagonjwa na mashine ya X-ray ili kupunguza usumbufu kwa wagonjwa wetu wanaosafiri umbali mrefu kwa huduma hizo,” aliongeza Dkt. Kombo.

Wakizungumza kwa niaba ya wenzao mara baada ya kupokea msaada huo, baadhi ya akinamama waliolazwa katika kituo hicho Zena Kikuji, Winfrida Sumpa, Lina Raphael na Tatu Bilal, waliishukuru Mwanga Marathon kwa moyo wa huruma waliouonyesha kwao.

“Tunawashukuru sana kwa kutujali,  msaada huu utatusaidia sana wakati wa kujifungua, Mungu awazidishie pale mlipopunguza,” walisema kwa pamoja akinamama hao kwa furaha.

Tukio hilo lilihudhuriwa pia na Diwani wa Kata ya Lembeni, Alex Josiah Mwipopo, aliyetoa wito kwa wadau mbalimbali wa maendeleo kuendelea kusaidia makundi yenye uhitaji maalum katika jamii.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.