MWANGA
Shirika la KIWAMWAKU Foundation linalojihusisha na utafiti wa mbegu za asili za mazao na miti, limeanzisha rasmi mradi maalum wa kuzitambua na kurejesha mbegu za asili zilizo hatarini kutoweka, kwa kushirikiana na wakulima na wadau wengine wa kilimo.
Akizungumza na waandishi wa habari wilayani Mwanga, Mkurugenzi wa Shirika hilo, Ezekiel Dembere, alisema mradi huo unalenga kufanya utafiti na uhifadhi wa mbegu za asili katika Kata za Kwakoa na Kigonigoni, zilizoko wilayani humo, ili kuhakikisha zinapatikana kwa wingi na kuendelea kuzalishwa kwa matumizi ya chakula cha asili nchini.
“Mbegu hizi zitaokotwa na kuhifadhiwa katika utaratibu mahsusi ambapo wakulima wataweza kuzipata kwa ajili ya kupanda tena shambani, tunataka kuona mbegu za asili zinarejea na kuchukua nafasi yake kama zamani,” alisema Dembere, ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya kilimo.
Shirika hilo lenye makao yake makuu wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro, linatekeleza mradi huu kwa ushirikiano na Shirika la Pelum Tanzania lenye makazi yake mkoani Morogoro.
Kwa mujibu wa Dembere, ushirikiano huo umewezesha watafiti wa mashirika yote mawili kupata mafunzo maalum juu ya mbegu za asili, kabla ya kwenda kufanya utafiti wa kina katika wilaya ya Chemba, mkoani Dodoma.
“Tulifanya utafiti wa mbegu za asili kama vile mtama, mahindi na alizeti, na kugundua kuwa mbegu hizo zimepungua kwa kasi kubwa kutokana na ujio wa mbegu za kisasa, hasa zile za kizazi cha GMO kutoka nje ya nchi, ambazo zinaathiri ustawi wa mbegu za asili,” alieleza.
Katika hatua nyingine, shirika hilo limeanza kampeni ya uhamasishaji katika Kata za Kigonigoni na Kwakoa, zilizopo wilayani Mwanga, kwa lengo la kutambua na kuhifadhi mbegu za asili kupitia uanzishwaji wa benki za mbegu zitakazosimamiwa na wakulima wenyewe.
“Tutatengeneza vikundi vya wakulima watakaopewa mafunzo ya namna ya kutambua mbegu za asili, kuzihifadhi, na kuzalisha kwa wingi ili zitumike sasa na kwa vizazi vijavyo,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Dembere, benki hizo za mbegu zitasaidia kuimarisha uhuru wa wakulima katika uzalishaji, na pia kulinda urithi wa chakula cha asili ambacho ni sehemu muhimu ya utamaduni wa Watanzania.
Akizungumza mmoja wa wakulima wa mahindi kutoka wilaya Siha mkoani hapa, Thomas Temu, alisema kuwa, mbegu za asili zimekuwa zikitumika tangu zamani kwa kilimo chenye tija.
"Mbegu za asili ni zile tunahifadhi baada ya kuvuna mazazo kwa ajili ya kilimo cha msimu unaofuata na hazina madhara yeyote." alifafanua mzee Temu.
Mkulima huyo alifafanua kuwa, mbegu za kisasa zilizalishwa kijenitikali (GMO seeds) huwezi kuzirudia kuzipanda tena baada ya kuvuna tofauti na zile mbegu za asili jambo ambalo limepelekea sisi wakulima kugeuka watumwa wa kununua mbegu kila msimu.
"Tunalipongeza sana shirika la KIWAMWAKU Foundation kwa kuja na utafiti huo ambao utatusaidia sisi wakulima kupatab mbegu za asili na kutupunguzia gharama kubwa ambazo tumekuwa tukitumia kwa ajili ya kununua mbegu za kisasa,"alisema Mzee Temu.








