BUNGENI-DODOMA.
Serikali imewataka wananchi kuacha kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo yanayozunguka Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, na imewahimiza kupanda miti kwa wingi ili kusaidia kuhifadhi mazingira na kuzuia kuyeyuka kwa barafu, hatua itakayosaidia kuendelea kuvutia watalii.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis, wakati akijibu maswali ya wabunge bungeni jijini Dodoma.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Moshi Vijijini, Prof. Patrick Ndakidemi, ambaye alitaka kufahamu kama Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha programu maalum za upandaji miti kutokana na kasi ya kuyeyuka kwa barafu ya Mlima Kilimanjaro, Naibu Waziri Khamis alieleza kuwa Serikali tayari imechukua hatua.
Alibainisha kuwa Serikali, kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, imeanzisha programu za upandaji miti katika maeneo ya milima, vilima na miinuko mbalimbali, sambamba na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira.
Aidha, aliwahimiza wananchi kupanda miti ya aina mbalimbali katika kila kaya, ikiwemo miti ya matunda, ili kuunga mkono juhudi za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kulinda mazingira kwa ujumla.




